2016-03-31 15:45:00

Msikubali kupokwa matumaini!


Askofu mkuu Eamon Martin wa Jimbo kuu la Armagh katika ujumbe wake kwa Mwaka Mpya wa 2016, ambao una umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa nchini Ireland, anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutokata tamaa na hatimaye, kutoa nafasi kwa wajanja wachache kuwapokonya matumaini ya maisha, kwani kwa kuendelea kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza katika maisha, kuna uwezekano mkubwa wa kuweza kuyashinda magumu na kuleta mabadiliko katika ulimwengu ambamo watu wengi wanaonekana kana kwamba, wamekata tamaa na kupoteza dira na mwelekeo wa maisha kwa siku za usoni.

Askofu mkuu Martin anaendelea kufafanua kwamba, kwa sasa watu wengi wanaendelea kuguswa na kutikiswa na vita vinavyoendelea sehemu mbali mbali za dunia kiasi hata cha kutishia Injili ya uhai; vitendo vya kigaidi ambavyo vinaendelea kusababisha hofu na mashaka kwa usalama wa raia na mali zao; umaskini wa hali na kipato, unaogumisha maisha ya watu wengi, kiasi hata cha kudhalilisha utu na heshima yao kama binadamu. Kuna baadhi ya viongozi wanaokiuka kanuni, sheria na maadili ya uongozi kiasi cha kuwa ni mzigo kwa raia na nchi zao pamoja na uwepo wa wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi.

Yote haya ni mambo ambayo yanaendelea kusababisha hofu na mashaka kwa watu wengi sehemu mbali mbali za dunia. Katika kipindi cha giza na hofu kuu, watu hawana budi kusikiliza Injili ya furaha, huruma, amani na matumaini, ili kufukuza giza la wasi wasi na hofu linalotanda katika mioyo na akili ya watu wengi. Athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimesababisha ukame sehemu mbali mbali za dunia na mafuriko ya kutisha kama ilivyojitokeza nchini Uingereza. Bado kuna Wakristo wanaoteseka na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Askofu mkuu Martin anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na moyo wa imani, matumaini na mapendo, pasi na kukata tamaa wala kuwaruhusu wajanja wachache kuwapokonya imani na matumaini yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wawe kweli ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na Injili ya furaha kwa wale wanaowazunguka, kwa kutambua kwamba, daima Kristo Yesu yu pamoja nao, tayari kuwasaidia kuleta mabadiliko katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Wakristo wanakumbushwa kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa matumaini ya Kikristo na kwamba, uwepo wao, unaweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu.

Waamini wawe tayari kuwashirikisha jirani zao Injili ya huruma na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake; hii furaha na matumaini baada ya kukutana na Kristo katika Neno, Sakramenti, Maisha na Sala. Kutokana na mwelekeo huu wa maisha mapya, Wakristo wawe tayari kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa kusikiliza kilio cha maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu na wanaishi duniani, nyumba ya wote.

Mwaka 2016, Ireland inafanya kumbu kumbu ya uhuru wao kutoka kwa Waingereza, kunako mwaka 1916, wakati huo, Vita kuu ya Kwanza ya Dunia ikiwa imepamba moto sehemu mbali mbali za dunia. Tukio hili linakuja wakati ambapo Mama Kanisa anaadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kumbe ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani; msamaha na upatanisho; ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Ni wakati wa kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo zinazofumbatwa katika upendo kwa Mungu na jirani; kwa kuheshimu, kuthamini, kutangaza na kushuhudia Injili ya maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Ni muda wa kujikita katika upatanisho wa kweli.

Matukio haya yote anasema Askofu mkuu Martin, yawasaidie waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushuhudia umuhimu wa kudumisha amani, utulivu na mshikamano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, daima wakiwa na matumaini kwa Kristo Yesu, Bwana na Mwokozi. Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni nafasi kwa waamini kumwilisna huruma ya Mungu katika maisha na vipaumbele vyao, huku wakionesha ari, mwamko na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.