2016-03-31 15:21:00

Kongamano la huruma ya Mungu Barani Ulaya!


Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kujikita katika toba, wongofu wa ndani na msamaha sanjari na kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu; Mjini Roma, kuanzia tarehe 31 Machi hadi 4 Aprili 2016 kunaadhimishwa Kongamano la Huruma ya Mungu kwa Bara la Ulaya. Hiki ni kipindi cha tafakari ya kina kuhusu dhana ya huruma ya Mungu; muda wa Sala na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu! Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni ushuhuda wa uwepo endelevu wa Kristo kwa waja wake.

Kardinali Christoph Schonborn, Rais wa  Kongamano la Kitume la Huruma ya Mungu Kimataifa katika tafakari yake ya ufunguzi kwa namna ya pekee amegusia huruma ya Mungu ambayo iliyomwilishwa tumboni mwa Bikira Maria; Kristo Yesu ambaye ni ufunuo wa huruma ya Baba wa milele katika maisha na utume na kwamba, huruma ni sehemu ya vinasaba vya asili ya binadamu. Huruma na haki ni chanda na pete anasema Kardinali Schonborn inayomwilishwa katika matendo kama anavyoonesha Yesu katika mfano wa Msamaria mwema, alipowalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili.

Huruma ya Yesu inaendelea kumwilishwa katika Ekaristi na Neno la Mungu. Waamini wanapaswa kukumbuka kwamba, huruma ya Yesu inapaswa kuwa ni mfano na kielelezo cha huruma yao kwa jirani zao kama Yesu alivyofanya kwa Bartimayo kipofu au yule mwanamke Msamaria aliyeomba huruma ya Yesu kwa ajili ya binti yake mgonjwa! Kilele cha huruma ya Yesu kinajionesha kwenye Fumbo la Msalaba, changamoto kwa waamini kutofanya mioyo yao migumu, ili waweze kuwa tayari kulipokea Neno la Mungu ambalo ni taa na dira katika maisha, vinginevyo huruma ya Mungu itawapitia kando!

Kardinali Schonborn anasema, Yesu alionesha huruma kwa wadhambi kama alivyofanya kwa yule Mwanamke Msamaria; kwani huruma na ukweli ni chanda na pete. Huruma inamrudishia mwamini maisha mapya, tayari kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma ya Mungu!

Kwa upande wake Padre Marcello Zubia, Mkuu wa Shirika la Wateatini amegusia kuhusu mashuhuda wa huruma ya Mungu katika historia, maisha na utume wa Kanisa. Hawa ni kama Mtakatifu Sebastiani aliyejitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwafariji wale waliokuwa wanateswa na kunyanyaswa, kiasi hata cha kuuwawa kikatili. Wengine ni akina Mtakatifu Giuseppe Maria Tomasi, mshauri wa ajabu kwa watu waliokuwa wamekengeuka katika misingi ya imani, maadili na utu wema. Mtakatifu Vincenti wa Pallotti ni mtakatifu aliyejisadaka kwa ajili ya umoja na mshikamano wa Kanisa kuzunguka Fumbo la Umwilisho wa Kristo! Kuna akina Sr. Maria Teresa Spinelli, Mtakatifu Marximilliano Maria Kolbe aliyejisadaka ili kukuza na kudumisha haki na umoja na hatimaye, Mtakatifu Fernando Rielo.

Wakati huo huo Padre Joseph Jost amefafanua dhana ya huruma na siasa kwa kuonesha jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu alijifunua kwa Musa pale Mlimani Sinai kwamba, Mungu ni mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira ni mwingi wa rehema na kweli. Hii ni changamoto ya kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu! Wanasiasa wanapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda na kudumisha mafao ya wengi; haki, amani na huduma ya mshikamano na usawa kati ya watu.

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, wanasiasa wanahamasishwa kuwa wahudumu makini wa huruma ya Mungu kwa watu wao, huku wakijitahidi kuwa kweli ni mashahidi wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; vyombo vya haki haki, amani na upatanisho wa kweli! Wanasiasa washuhudie huruma ya Mungu katika maisha ya hadhara, kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema.

Kwa upande wake, Tori Mcclure, Rais wa Chuo Kikuu cha Louisville, Kentucky, Marekani, amegusia mtandao wa miji yenye huruma duniani, akikazia umuhimu wa huruma kama chachu ya kuondokana na woga na chuki zisizokuwa na mashiko wala mvuto kwa maendeleo ya watu; huruma inayowaondoa watu kutoka katika mashindano na uchoyo na kwamba, huruma haina kipimo! Haya ni mambo msingi ambayo Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuyapatia umuhimu wa pekee wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.