2016-03-31 16:10:00

Kanisa linatangaza Ujumbe wa Matumaini!


Kanisa katika kipindi hiki cha Pasaka linapomshangilia Kristo Mfufuka, linaendelea kuombea amani katika Nchi Takatifu na Mashariki ya Kati katika ujumla wake; linaguswa na mahangaiko pamoja na mateso ya wakimbizi na wahamiaji kutoka mashariki ya Kati; linaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuonesha moyo wa upendo na ukarimu; utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa wakimbizi na wahamiaji. Haya ndiyo mambo makuu ambayo yanafumbatwa katika Ujumbe wa Pasaka uliotolewa na viongozi wa Makanisa Nchi Takatifu.

Huu ni ujumbe wa kiekumene uliotiwa sahihi na viongozi wa Makanisa huko Nchi Takatifu. Viongozi hawa wanasema, Kanisa limejiandaa kwa muda wa Siku 40 za Kipindi cha Kwaresima, kwa kufunga, kusali, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma; sasa linamshangilia Kristo Mfufuka. Mateso na mahangaiko ya binadamu yanageuzwa kuwa ni chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba, mahali ambapo huruma na upendo wa Mungu vinakutana na kuambatana.

Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, Yesu ameshinda dhambi na mauti, kaburi wazi mjini Yersalemu ni kielelezo cha umwilisho wa matumaini yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya viumbe wote. Pasaka ya Bwana ni tukio la ukombozi linalowagusa watu wote pasi na ubaguzi! Hii ni changamoto ya kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa kujenga madaraja ya watu kukutana na kusaidiana.

Viongozi wa Makanisa wanasema, kuta za utengano hazina mashiko wala mvuto kwa ustawi na maendeleo ya wengi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kuta hizi ni  chanzo cha utengano na kinzani za kijamii; ukosefu wa maridhiano kati ya watu pamoja na watu kutopokeana kama ndugu. Jumuiya ya Kimataifa inahitaji mashuhuda na wajenzi wa madaraja yatakayoimarisha na kudumisha: maridhiano, urafiki, udugu na ukarimu; mambo msingi yanayoweza kusaidia kutoa faraja kwa watu wanaoteseka na kunyanyasika kwa kulazimika kuyakimbia makazi yao!

Viongozi wa Makanisa wanawakumbuka na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria, ili kweli mwanga wa Kristo Mfufuka uweze kung’ara tena katika akili na nyoyo za wananchi wanaoteseka, na hivyo Jumuiya ya Kimataifa kuweza kuguswa na mateso ya watu hawa tayari kuibua mbinu mkakati wa kuwasaidia kuweza kupata tena amani na utulivu. Mbiu ya Pasaka haina maana sana kwa watu wanaoishi katika Nchi Takatifu, ikiwa kama hakuna haki, amani na maridhiano kati ya watu. Yerusalemu ni mji wa matumaini ya Fumbo la Ufufuko kwa nchi Takatifu na Ulimwengu katika ujumla wake.

Viongozi wa Makanisa huko Nchi Takatifu wanahitimisha ujumbe wao wa kiekumene kwa Familia ya Mungu kwa kusema, matumaini yao makubwa yanajikita katika msingi wa haki na amani ya kudumu huko Nchi Takatifu na Mashariki ya Kati katika ujumla wake. Mji wa Yerusalemu unapaswa kuishi katika amani; mahali ambapo Watu wa Mungu wanaweza kuishi katika umoja, amani, udugu na mshikamano, huku wakiheshimiana na kuthaminiana. Mwenyezi Mungu ameupatanisha ulimwengu wote pamoja naye kwa njia ya Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo. Wakristo wote wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya upatanisho, kwani wao ni mabalozi wa Kristo sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.