2016-03-30 08:56:00

Wanawake Barani Afrika wana mchango mkubwa katika kudumisha amani!


Askofu mkuu Bernadito Auza, mwakilishi wa kudumu wa VaticanĀ  kwenye Umoja wa Mataifa anasema, Kanisa linatambua mchango mkubwa unaotolewa na wanawake katika medani mbali mbali za maisha, hususan katika familia na maisha ya kiroho; diplomasia, katika mchakato wa utunzaji na udumishaji wa amani duniani. Ajenda ya Maendeleo endelevu kwa mwaka 2030 haitaweza kupata mafanikio makubwa, ikiwa kama wanawake kutoka Barani Afrika hawatahusishwa kikamilifu.

Askofu mkuu Auza alikuwa anachangia hoja kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mjadala wa wanawake, amani na usalama, uliofanyika hivi karibuni huko New York, Marekani. Amani, maendeleo na ushirikishwaji wa wengi bado ni ndoto kwa nchi nyingi zilizoko kwenye Ukanda wa Maziwa makuu, Barani Afrika, lakini wanawake wanaweza kuchangia katika kufanikisha mchakato wa kudumisha amani.

Wanawake wakijengewa uwezo wanaweza kuwa kweli vyombo vya kidiplomasia katika kuzuia, kupatanisha, kushiriki na kuhamasisha mchakato wa ujenzi wa amani duniani; changamoto ambayo inapaswa kumwilishwa katika vitendo, ili kuzuia kinzani na mipasuko ya kijamii; kujenga na kuimarisha amani. Wanawake wana uwezo mkubwa katika kuwaelimisha watu kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya jirani zao pamoja na kukazia mchakato wa upatanisho mara baada ya vita na kinzani mbali mbali.

Ujumbe wa Vatican unawapongeza wanawake kwa kujitoa bila ya kujibakiza katika huduma kwenye sekta ya elimu, afya na malezi ya vijana wa kizazi kipya. Lakini kwa bahati mbaya, wanawake na wasichana wamekuwa ni wahanga wa nyanyaso na dhuluma za kijinsia wakati wa vita na kinzani za kijamii. Askofu mkuu Auza ametambua mchango uliokuwa unatolewa na Watawa wa Shirika la Mama Theresa wa Calcutta nchini Yemen waliouwawa kikatili hivi karibuni, bila kumsahau Padre Tom aliyeuwawa kikatili siku ya Ijumaa kuu. Baba Mtakatifu akirejea kwenye matukio haya amesikika akiwataka wahusika wote kuweka silaha zao chini na kuanza kujikita katika mchakato wa majadiliano na kwamba, damu ya mashuhuda hawa wa imani itasaidia kukoleza mchakato wa haki, amani na upatanisho nchini Yemeni.

Wanawake wengi Barani Afrika wameendelea kuwa mstari wa mbele kuwatetea watu wasiokuwa na sauti; wamesimama kidete kuzuia mipasuko ya kijamii; wamewakuwa ni msaada mkubwa kwa waathirika wa vita; watetezi makini wa utu na haki msingi za binadamu. Vatican inapania kuimarisha na kuendeleza mchakato wa kuwajengea uwezo wanawake Barani Afrika, ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa amani na jamii shirikishi. Uwepo wa wanawake wengi katika medani za kisiasa na kidiplomasia unaweza kuchangia katika kukuza mchakato wa maendeleo endelevu na amani!

Elimu ni nyenzo msingi ili kuwajengea wanawake uwezo, ili hatimaye, waweze kushiriki kikamilifu kuchangia ustawi na maendeleo ya watu wao. Kanisa Katoliki Barani Afrika, limekuwa mstari wa mbele katika kuchangia elimu bora na makini sanjari na kuwajengea uwezo wasichana ili kuwainua. Hata hivyo, Askofu mkuu Auza anakiri kwamba, bado kuna umati mkubwa wa wanawake wanaodhulumiwa na kunyanyaswa, wanaotengwa na kutelekezwa.

Ubakaji umekuwa ukitumiwa na baadhi ya wanajeshi kwenye maeneo ya vita kama silaha; ni watu wanaonyanyaswa kwenye kambi za wakimbizi na wahamiaji; wanatumbukizwa katika utumwa mamboleo sanjari na biashara haramu ya binadamu na utalii wa ngono! Ni watu wanaokumbana na ukatili wa utoaji mimba, ndoa na wongofu wa shuruti. Haya ni matukio ambayo yanaendelea kuongezeka maradufu katika uso wa dunia badala ya kutoweka. Ni matukio yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.