2016-03-30 09:24:00

Wananchi wa Sudan ya Kusini wanataka amani!


Viongozi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni nchini Sudan ya Kusini, wanasema, viongozi wa kisiasa nchini humo wanapaswa kuonesha utashi wa kisiasa kwamba wanataka kumaliza mgogoro wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan ya Kusini, vita ambayo imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao! Watu wamechoka kusikia matamko ya kisiasa ambayo hayatekelezwi na matokeo yake wananchi wanaendelea kuteseka kutokana na vita.

Sudan ya Kusini, moja ya mataifa machanga kabisa Barani Afrika kwa miaka ya hivi karibuni, imekuwa ni uwanja wa fujo na ghasia, kiasi cha kuhatarisha amani, usalama na mafungamano ya kijamii kati ya wananchi wa Sudan ya Kusini ambao kwa sasa wanafikia millioni kumi na mbili! Viongozi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni nchini Sudan katika ujumbe wao wa Kipindi hiki cha Pasaka wanakaza kusema, Sudan inahitaji kuona misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa ikipewa kipaumbele cha pekee.

Kila mtu akichangia kadiri ya uwezo na nafasi yake, historia ya Sudan inaweza kubadilika kutoka katika vita na kinzani na kuanza kuambata mchakato wa haki, amani na maridhiano ya kitaifa. Wananchi wanataka kuandika historia ya amani, kwani wamechoka na vita! Kwa njia ya majukwaa ya kidini, viongozi wa Makanisa wanapenda kuwashirikisha wadau mbali mbali katika mgogoro wa kivita Sudan ya Kusini, ili kujadili na kuona sababu za vita kuendelea kuwepo nchini Sudan licha ya mikataba ya amani kutiwa sahihi kwa mashangilio makubwa?

Viongozi wa kidini Sudan ya Kusini wanakaza kusema, hatima ya Sudan ya Kusini iko miokononi mwa wanawanchi wenyewe. Askofu mkuu Paulino Lukudu Loro wa Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini anasema, umefika wakati wa kujifunga kibwebwe ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Sudan ya Kusini.Haiwezekani kuendelea kushuhudia watoto wakifariki dunia kutokana na utapiamlo wa kutisha; na watu kuendelea kunyanyasika katika nchi yao wenyewe! Wananchi wanataka kuona mwanga wa Kristo Mfufuka katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.