2016-03-29 10:32:00

Utunzaji bora wa mazingira kama tendo la huruma!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni fursa muafaka kwa Familia ya Mungu kutafakari tena na tena kuhusu matendo ya huruma kiroho na kimwili kama namna bora zaidi ya kumwilisha huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu. Hivi karibuni, Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, akiwa kwenye Chuo kikuu cha Villanova, huko Philadelphia, Marekani alitoa tafakari kuhusu utunzaji bora wa mazingira kama tendo la huruma linaloonesha uhusiano wa pekee kati ya Mungu, mwanadamu na kazi ya Uumbaji.

Katika tafakari yake, Kardinali Turkson amefafanua maana ya kazi ya Uumbaji; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, mintarafu changamoto zinazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji, Laudato si; fadhila ya huruma na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Mambo yote haya ni kuwawezesha waamini kuadhimisha kikamilifu Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kadiri ya mazingira yao, huku wakitambua kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu hata katika kulinda na kutunza mazingira bora.

Kardinali Turkson anakaza kusema, zawadi ya maisha ya mwanadamu inafumbatwa katika mahusiano ya mambo makuu matatu: kwanza ni Mwenyezi Mungu ambaye ni chemchemi ya uhai wa mwanadamu; pili ni mwanadamu mwenyewe aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu anayepaswa kuwa na mahusiano mema na jirani zake na tatu na dunia ambayo kimsingi ni kazi ya Uumbaji iliyofanywa na Mwenyezi Mungu na akamkabidhi binadamu ili aweze kulinda, kuitunza na kuiendeleza. Hapa inasikitisha kuona kwamba kazi nyingi za binadamu zimekuwa ni chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira, leo hii athari za mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kwani ni chanzo kikuu cha maafa na umaskini kati ya watu.

Kardinali Turkson anafafanua kwamba, huruma ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa; hapa watu wanaonja huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa kwa namna ya pekee katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kwa njia hii, Familia ya Mungu inakutana na Kristo kwa kuwalisha wenye njaa; kuwanywesha wenye kiu; kuwavika walio uchi; kuwakaribisha wageni; kuwatembelea na kuwafariji wagonjwa; kuwatembelea na kuwahudumia wafungwa; kuwazika wafu kwa heshima na ibada. Matendo ya huruma kiroho ni pamoja na kuwashauri wenye shaka; kuwafundisha wajinga; kuwaonya wakosefu; kuwafariji wenye huzuni; kusamahe makosa; kuwavumilia wasumbufu pamoja na kuwaombea wazima na wafu.

Kardinali Turkson anasema katika mazingira yote haya, mwamini anakutana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya jirani zake. Matendo haya ya huruma yanafumbatwa kwa namna ya ajabu katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, Laudato si, na hapa mkazo ni utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Hapa mwaliko ni kwa Familia ya Mungu kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na kile kijacho. Kila mwamini katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ajibidishe kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira bora katika maeneo yake. Changamoto hii inakwenda sanjari na mapambano dhidi ya njaa, umaskini na magonjwa; uchafuzi wa mazingira na ukosefu wa fursa za ajira. Haya ni mambo yanayogusa utu na heshima ya binadamu! Mwaka wa huruma ya Mungu unatoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu aliyeasili ya huruma na mapendo kwa binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.