Baraza la Maaskofu Katoliki Canada katika ujumbe wake wa Kipindi hiki cha Pasaka, linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu, kwa kuonesha huruma na mapendo kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao.
Kwa namna ya pekee, katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, waamini wanaalikwa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha, kama sehemu ya mkakati wa kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu sanjari na utakatifu wa maisha ya binadamu, tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu!
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linasema, Kanisa linatangaza Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo na kwa njia hii waamini wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Msalaba! Maaskofu wanawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kuwaangalia wakimbizi na wahamiaji wanaoteseka; watu wanaotembea mwendo mrefu ili kutafuta hifadhi na usalama wa maisha yao; ni makundi makubwa ya watu wanaokimbia vita, nyanyaso, dhuluma, umaskini na kinzani za kijamii.
Wakimbizi hawa kwa sasa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi kwenye kambi ambazo zimefurika kupita kiasi. Kuna watoto ambao wamepotezana na wazazi na walezi wao kutokana na vita kumbe, wote hawa wanapaswa kuonjeshwa huruma na mapendo. Hii ni changamoto anasema Askofu Douglas Crosby, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Canada kuonesha huruma na upendo, kwa kuchangia kwa hali na mali katika mchakato wa kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji.
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linakaza kusema, Kanisa limetoa baadhi ya miundo mbinu yake kwa ajili ya kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji. Baadhi ya wakimbizi na wahamiaji wameanza kuonja huruma na ukarimu wa waamini wa Canada, mwaliko kwa waamini kuendelea kufuata nyayo za Kristo Mfufuka, kwa kutangaza na kushuhudia nguvu ya upendo na huruma ya Kristo Mfufuka kwa watu wanaoteseka, ili waweze kuwa na maisha mapya!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©. |