2016-03-29 10:46:00

Mwaka wa huruma ya Mungu na Majadiliano ya kidini!


Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Shirisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki, Caritas Internationalis anasema, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mem wanaweza kushirikiana na kushikamana kikamilifu katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu na mazingira yao.

Huu ni mwaliko pia wa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu; huduma makini na mshikamano dhidi ya umaskini pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni mambo msingi kabisa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia! Haya ni kati ya mambo ambayo yamechambuliwa na Kardinali Tagle wakati wa uzinduzi wa kitabu kuhusu “Dini na Siasa”, kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Gregorian kilichopo mjini Roma. Kitabu hiki ni matokeo na mchango wa shule ya Sinderesi iliyoko kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Gregoriana.

Kardinali Tagle anawataka wanafunzi kujifunza somo la dini si tu katika nadharia inayobaki ikielea katika ombwe, bali somo la dini, liwasaidie kufahamiana, kuheshimiana na hatimaye, kujenga urafiki na udugu, tayari kufanya mang’amuzi ya maisha kwa kuonja na kushiriki maisha, dini na tamaduni za watu wengine, jambo ambalo litawawezesha wanafunzi hao kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa maisha. Imani na tamaduni ni mambo yanayofumbatwa katika maisha ya watu.

Hapa kuna haja ya kukudumisha ukomavu wa akili kitamaduni, ili kujifunza, kufahamu na kuthamini imani na dini za watu wengine. Waamini wajifunze tofauti zao na pale ambapo wanakutanika na kushikamana kama Familia ya Mungu. Hii ni changamoto kwa vijana wa kizazi kipya kukuza na kudumisha akili ya kitamaduni, ili kujenga msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni dhana inayopatikana katika dini zote, kumbe hata waamini wa dini mbali mbali wanaweza kuwasaidia Wakristo kujifunza dhana ya huruma ya Mungu na kwa njia hii, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yatakuwa na utajiri mkubwa zaidi. Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwataka Wakristo kujikita zaidi na zaidi katika mchakato wa majadiliano ya kidini.

Kurasa nyingi za Agano la Kale zinasheheni huruma na upendo wa Mungu. Vitabu vitakatifu vya dini ya Kiislam vinamwonesha Mungu kuwa ni mwenye huruma na mpole; anayewasindikiza binadamu katika safari yao ya maisha na kwamba, huruma yake haina mipaka! Kwa namna ya pekee anakaza kusema Kardinali Tagle, Wakristo wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa waja wake, hususan wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Ni huruma inayoshuhudiwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; tayari kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima, haki, amani na upatanisho. Wahanga wa nyanyaso na ukosefu wa haki msingi za binadamu, hawajaoneshwa huruma, kumbe, hawa wapewe kipaumbele cha pekee.

Utajiri wa huruma ya Mungu unaofumbatwa katika dini mbali mbali ushuhudiwe, ili kujenga jamii inayojikita katika upendo na mshikamano wa dhati. Familia ziwe ni shule ya huruma ya Mungu inayomwilishwa kila siku ya maisha na kwamba, waamini wa dini mbali mbali washinde kishawishi cha misimamo mikali ya kidini na kiimani, ili kweli haki, amani na maridhiano viweze kutawala katika akili na nyoyo za watu. Waamini wa dini mbali mbali wajenge utamaduni wa kukutana na kushirikiana kutoa huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, hususan wakimbizi na wahamiaji ambao kwa sasa wanaonekana kuwa ni “kero kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa”.

Mateso na mahangaiko ya watu liwe ni daraja la umoja na mshikamano wa huruma na mapendo bila kuwasahau wale wanaoteseka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Waamini wa dini mbali mbali hawana budi kushikamana na kushirikiana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi; kwa kukuza misingi ya haki, amani na maridhiano ya kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.