2016-03-29 09:58:00

Kristo Mfufuka ni chemchemi ya haki, amani na upatanisho!


Waamini wanakumbushwa kwamba, wameoshwa dhambi zao kutoka kwa Mwanakondoo wa Mungu; Kristo Yesu aliyesulubiwa pale Msalabani, amefufuka kwa wafu na hivyo kushinda dhambi na mauti kwa njia ya upendo, huruma na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa njia ya Fumbo la Pasaka, Yesu amewapatanisha walimwengu wote na Baba yake wa mbinguni na kwa njia ya mateso na kifo chake, mwanadamu ameweza kukombolewa!

Huu ndio ujumbe wa Pasaka ambao Mama Kanisa anaona fahari kuutangaza na kuushuhudia wakati huu wa maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka ya Bwana! Hiki ni kipindi cha imani, matumaini na mapendo; changamoto na mwaliko wa kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka anayeendelea kutenda kazi katika historia ya maisha ya mwanadamu. Yesu anatangaza uhuru kwa wale wote waliosetwa katika kongwa la utumwa wa dhambi; Kristo ni tumaini la wale wote wanaoteseka na kudhulumiwa kwa ajili ya imani na uaminifu wao kwa Kristo na Kanisa lake! Hii ndiyo imani inayoendelea kuwaimarisha kwamba, iko siku wataweza hata wao kufufuka na Kristo Yesu.

Hivi ndivyo anavyoandika Kardinali Charles Maung Bo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu Yangon, nchini Myanmar ambayo kwa sasa inamwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuwaletea ukombozi wa kisiasa, kiuchumi na kijamii, mwaliko kwa wananchi wa Myanmar kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Miaka 50 imekuwa ni ya shida na mateso makubwa kwa wananchi wengi wa Myanmar, lakini sasa wanaanza kuona mwanga wa matumaini mapya baada ya kufanikisha uchaguzi na cheche za demokrasia kuanza kutawala tena! Hiki ni kipindi cha kuponya machungu na madonda ya ndani yaliyosababishwa na utawala dhalimu; ni fursa ya kukuza amani, ustawi na maendeleo ya wengi!

Mama Kanisa anashangilia na kushuhudia ushindi wa Kristo Mfufuka aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Msalaba umekuwa ni mti wa ukombozi na chemchemi ya maisha mapya na kwa njia ya madonda yake, mwanadamu ameweza kupona! Maadhimisho ya Pasaka ya Bwana katika kipindi cha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni wakati muafaka wa kujipatanisha na Mungu, jirani na mazingira kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Waamini wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa waja wake.

Wakristo wawe ni alama ya matumaini kwa jirani zao. Kanisa nchini Myanmar, limejizatiti kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa nchi kwa kuchangia katika mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa, chachu muhimu sana katika kukuza na kudumisha maendeleo ya watu: kiroho na kimwili sanjari na kusimamia haki msingi za binadamu. Ni wajibu wa wananchi wote kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; wawasaidie wakimbizi na wahamiaji kupata huduma msingi, ili kweli nchi hii iweze kuwa ni alama ya haki, amani na upatanisho kati ya watu! Kanisa litaendelea kutoa elimu makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani elimu ni ufunguo wa maisha bora kwa wengi!

Waamini waoneshe pia huruma, upendo na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukimizwa pembezoni mwa jamii, kwa kuwatangazia Injili ya furaha na matumaini kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Baada ya Ijumaa kuu, sasa Wakristo wanapaswa kumshuhudia Kristo Mfufuka, kwani wao ni watu ambao kwa sasa wanatembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka! Na kwa maneno haya Kardinali Charles Maung Bo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu laYangon nchini Myanmar anakamilisha ujumbe wake wa Pasaka kwa Mwaka 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.