2016-03-29 15:03:00

Askofu mkuu Mouradian apongezwa na Papa kwa Jubilei ya miaka 25 ya Uaskofu


Baba Mtakatifu Francisko amempongeza Askofu mkuu Kissag Mouradian mkuu wa Kanisa la Waarmeni nchini Argentina na Chile kwa kuadhimisha Jubilei ya miaka 25 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake wa matashi mema, anapenda kuungana na Familia ya Mungu nchini Argentina na Chile kwa kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya Daraja Takatifu alilokirimiwa Askofu mkuu Mouradian.

Baba Mtakatifu anamtakia heri na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa mema yote aliyokwisha kutenda katika kipindi hiki cha miaka 25 na yale atakayoendelea kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu kwa siku za usoni! Ujumbe wa Baba Mtakatifu umesomwa wakati wa maadhimisho ya Jubilei hii iliyofanyika hapo tarehe 22 Machi 2016 huko Argentina. Baba Mtakatifu anamwombea Askofu mkuu Mouradian, ili Yesu Kristo aendelee kumwezesha kupata mafanikio mengi zaidi pamoja na kumweka Askofu mkuu na familia ya nzima ya Mungu huko Argentina na Chile chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria.

Jumuiya ya Waarmeni kutoka Argentina inafafanua kwamba, ujumbe huu ni kielelezo cha mwendelezo wa urafiki kati ya Baba Mtakatifu Francisko tangu alipokuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires. Viongozi mbali mbali wa Kanisa nchini Argentina wamewasilisha salam na matashi mema kwa Askofu mkuu Kissag Mouradian anapomwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa Jubilei ya miaka 25 ya kuwekwa wakfu kama Askofu!. Sherehe hii imehudhuriwa pia na viongozi mbali mbali wa dini na serikali nchini Argentina!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.