2016-03-28 08:43:00

Wakimbizi na wahamiaji waangaliwe kwa jicho la huruma!


Askofu Titus Joseph Mdoe wa Jimbo Katoliki Mtwara katika mahojiano maalum na Radio Vatican anapenda kuliangalia tatizo na changamoto ya wakimbizi na wahamiaji kwa jicho la huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu! Leo hii kuna mfumuko mkubwa wa wahamiaji na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora ugenini! Makundi makubwa ya watu hawa ni wale wanaokimbia vita, umaskini, dhuluma, nyanyaso na mipasuko ya kidini, kijamii na kisiasa.

Ni watu wanaokimbia majanga na maafa katika nchi zao, kumbe hawa ni watu wanaohitaji kwanza kabisa kuonjeshwa huruma na upendo na hatimaye, kupewa msaada wanaohitaji, kwa kuzingatia: haki msingi, heshima na utu wao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu! Jamii inapaswa kuwajali na kuwaonesha mshikamano wa upendo huko wanaotafuta hifadhi ya maisha! Wakimbizi na wahamiaji kwa sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa, kwani inaonekana kana kwamba, watu wamechoka na hawataki tena kuwaona wala kuwasaidia.

Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji, huku wakiwa na sera na mikakati inayotekelezeka. Na mambo haya anasema Askofu Mdoe yanapaswa kuamriwa na kutekelezwa kwa umoja na ushirikiano vinginevyo, itakuwa vigumu kwa baadhi ya nchi kuweza kubeba uzito wote wa changamoto na matatizo ya wakimbizi na wahamiaji duniani. Nchi majirani nao waoneshe mshikamano kwa kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji kwa hali na mali!

Askofu Titus Joseph Mdoe anakaza kusema, lakini haitoshi kuwapokea na kuwapatia hifadhi wakimbizi na wahamiaji, bali kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta suluhu ya kudumu ya vyanzo vya matatizo na changamoto zinazopelekea makundi makubwa ya watu kukimbia au kuhama nchi zao! Kwani hapa si bure kuna sababu msingi! Uzoefu na mang’amuzi yanaonesha kwamba, wengi wa wakimbizi na wahamiaji ni wale wanaotoka katika maeneo yenye vita, migogoro na kinzani za aina mbali mbali! Ni watu wanaokimbia umaskini, majanga asilia, nyanyaso, dhuluma na ukosefu wa haki msingi za binadamu!

Haya ni mambo yanayopaswa kushughulikiwa kwanza kabisa na Serikali husika kwa kukuza na kudumisha utawala wa sheria, uhuru wa kuabudu na haki msingi! Jumuiya ya Kimataifa nayo haina budi kuhakikisha kwamba, mambo haya yanatekelezwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi! Mambo haya yakipewa ufumbuzi wa kudumu anasema Askofu Mdoe, tatizo la wakimbizi na wahamiaji linaweza kupatiwa ufumbuzi.

Siasa kali, misimamo mikali ya kidini na kiimani na mipasuko ya kidini ni mambo yanayozalisha pia makundi ya kigaidi ambayo kwa sasa yamekuwa ni hatari kwa Jumuiya ya Kimataifa. Hapa kuna haja ya kuwekeza katika elimu makini, fursa za ajira kwa vijana kwani hakuna mtu ambaye anazaliwa akiwa gaidi! Hawa ni watu wanaobeba ndani mwao machungu mazito ya maisha! Kumbe, hapa Jamii inapaswa kuyafahamu machungu haya ili kuyapatia ufumbuzi wa kudumu kwa njia ya upendo na mshikamano, badala ya kuwatenga na kuwajengea chuki na kisasi! Huruma ya Mungu inayojionesha katika haki!

Askofu Titus Mdoe wa Jimbo Katoliki Mtwara, Tanzania anahitimisha mahojiano maalum na Radio Vatican kwa kusema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni nafasi ya kukabiliana na changamoto na tatizo la wakimbizi kwa jicho la huruma ya Mungu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko, ili kweli waweze kutambua kwamba, dunia inawajali na kuwathamini na kwamba, inataka kuyashughulikia matatizo na changamoto za maisha yao kwa njia ya mshikamano wa upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.