2016-03-28 14:36:00

Vitendo vya kigaidi vinapandikiza chuki na uhasama mioyoni mwa watu!


Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, Jumatatu tarehe 28 Machi 2016 aliyaelekeza mawazo yake Jimbo kuu la Lahore, nchini Pakistan, ambako wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka, shambulizi la kujitoa mhanga lilisababisha watu 70 kufariki dunia na wengine 340 kujeruhiwa vibaya, wakati walipokuwa wanaadhimisha Siku kuu ya Pasaka. Baba Mtakatifu ametumia nafasi hii kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wote walioguswa na maafa haya makubwa.

Anaendelea kuwaombea waliopoteza maisha, ili waweze kupata faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anawasihi viongozi wa Serikali na wale wote waliopewa dhamana kijamii kuhakikisha kwamba wanadumisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao, hususan waamini wa makundi madogo madogo. Baba Mtakatifu anarudia kusema, mauaji na chuki yanapelekea machungu mioyoni mwa watu na uharibifu mkubwa lakini heshima, udugu na umoja ni mambo muhimu sana katika kukuza na kudumisha misingi ya amani.

Maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka yasaidie kuchochea ari na sala zaidi kwa Mwenyezi Mungu, ili aweze kuzuia watu wenye mikono ya chuki na uhamasa, wanaopandikiza hofu, wasi wasi na kifo, ili dunia iweze kutawaliwa na amani, haki na upatanisho. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia waamini na mahujaji wote heri na baraka, amani na utulivu katika maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka. Kipindi hiki iwe ni fursa nyingine tena ya kusoma na kulitafakari Neno la Mungu, sehemu zile zinazozungumzia Ufufuko wa Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.