2016-03-28 09:02:00

Nigeria inapaswa kupyaisha maisha yake ya kiroho!


Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria anasema, changamoto za kimaadili, kiuchumi, kisiasa na kijamii zinazoikabili Nigeria zinaweza kupewa kisogo, ikiwa kama Familia ya Mungu nchini Nigeria itajikita katika mchakato wa kupyaisha maisha yake ya kiroho, kiutu na kijamii. Hapa lazima ijikite katika kanuni maadili, utu wema, umoja na mshikamano wa kitaifa, tayari kusimama kidete kulinda na kutetea mafao, ustawi na maendeleo ya wengi badala ya mwelekeo wa sasa wa watu kujitafuta wenyewe na matokeo yake ni ubinafsi, uchu wa mali na madaraka!

Nigeria kwa sasa haina budi kujifunga kibwebwe ili kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa na ukosefu wa ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Hii ni changamoto kwa familia ya Mungu nchini Nigeria kushirikiana kwa karibu zaidi na Serikali ili kuhakikisha kwamba, majanga haya yanapatiwa ufumbuzi wa kudumu. Familia ya Mungu ikitumia silaha za maisha ya kiroho; toba na wongofu wa  ndani; sala na kufunga; inaweza kuvuna matunda yanayokusudiwa, yaani haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi.

Matatizo mengi ya wananchi wa Nigeria yanatokana na kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema; changamoto ya kutubu na kumwongokea Mungu; tayari kuambata msamaha na huruma yake. Saratani ya rushwa na ufisadi imepelekea ukosefu wa haki, amani, usalama na maridhiano kati ya wananchi wa Nigeria. Leo hii Nigeria inatambulikana zaidi kutona na vitendo vya kigaidi. Rushwa na ufisadi, vimeendelea kunenepesha mifuko ya wananchi wachache, wakati mamillioni ya watu yanaendelea kuteseka kwa umaskini, ujinga na maradhi. Leo hii Nigeria imeshuka kimaendeleo kwa sababu ya uchu wa mali na madaraka.

Kanisa kwa miaka mingi limekuwa mstari wa mbele kupambana na saratani ya rushwa kwa kuwataka waamini na wananchi wa Nigeria kufanya toba na wongofu wa ndani; kwa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Haki itaweza kudumishwa Nigeria ikiwa kama watu watakuwa na hofu ya Mungu na upendo kwa jirani. Upyaisho wa maisha ya kiroho; maadili na utu wema; umoja na mshikamano wa kitaifa ni mambo msingi katika mchakato wa mabadiliko nchini Nigeria. Familia ya Mungu nchini humo haina budi kuthubutu: kutubu, kusamahe na kujipatanisha.

Kardinali Onaiyekan anasikitika kusema kwamba, mapambano ya kigaidi sanjari na mashambulizi yanayofanywa na Boko Haram yamepelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao. Serikali imewekeza fedha nyingi ya umma katika kununua silaha, lakini bado wananchi wengi wanaendelea kupoteza maisha na mali zao. Wapiganaji wa vikosi vya kigaidi si wageni kutoka nje ya Nigeria, hawa ni watoto wa Nigeria, kumbe, kuna haja ya kuwahamasisha kuacha njia yao mbaya na kuanza mchakato wa kuwa ni sehemu ya maisha ya wananchi wa Nigeria, ili kukuza na kudumisha haki, amani, ustawi na maridhiano kati ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.