2016-03-28 11:40:00

Muasisi wa EWTN, Mama Angelica amefariki dunia!


Mama Mary Angelica wa Shirika la Watawa wa Kupashwa habari kuzaliwa kwa Bwana, P.C.P.A, mwanzilishi wa mtandao wa vituo vya Televisheni vya Kanisa Katoliki, EWTN amefariki dunia, Jumapili ya Pasaka, tarehe 27 Machi 2016 akiwa na umri wa miaka 92, huku akiwa amezungukwa na watawa wenzake. Mama Angelica atakumbukwa sana na wengi kwa kuasisi mtandao wa televisheni za Kanisa Katoliki nchini Marekani.

Ni mtawa ambaye hata katika mateso na mahangaiko yake ya ndani bado alionesha furaha na maisha ya sala huku akijikita katika tasaufi ya Mtakatifu Francisko wa Assis katika uhalisia wa maisha yake! Itakumbukwa kwamba, alizaliwa kunako mwaka 1923 huko Ohio, Marekani. Baada ya majiundo yake ya kitawa, akaweka nadhiri za daima mwezi Januari 1953 kama Mtawa wa Mtakatifu Clara, mkaa pweke! Kunako mwaka 1980 Mama Angelica akajimwaga katika uwanja wa mawasiliano ya jamii kwa kugeuza gereji ya jumuiya yake kuwa ni Studio ya kuandalia vipindi vya televisheni na huo ukawa ni mwanzo wa “Eternal World Televishen Network (EWTN).

Tarehe 15 Agosti 1981akaanzisha mtandao wa televisheni ya Kikatoliki na kutegemea ufadhili kutoka kwa watazamaji wake, kiasi hata cha kuhatarisha kufilisika kwa kituo hiki, lakini ni mtawa aliyekuwa anamtumainia sana mwenyezi Mungu. Matangazao yake yakasambaa na kuwafikia watu zaidi ya millioni 264 katika mchi 145. Mtawa huyu akawa maafuru sana katika kufundisha imani ya Kanisa Katoliki. Kunako mwaka 2000 akang’atuka kutoka madarakani na kutangazwa kuwa ni kati ya watawa maarufu sana ndani ya Kanisa Katoliki nchini Marekani.

Mama Angelica ni mtawa ambaye amepambana sana na magonjwa katika maisha yake pasi ya kukata wala kukatishwa tamaa. Kunako mwaka 2009 Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akatambua mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa na kumpatia nishani ya kipapa “Pro Ecclesia et Pontifice”. Baba Mtakatifu Francisko mwezi Februari, 2016 akiwa njiani kuelekea Cuba, alimtumia ujumbe wa matashi mema na kumwomba ili amsindikize katika hija yake ya kitume nchini Mexico, lakini kwa namna ya pekee, alipokuwa anajiandaa kukutana na kuzungumza na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima! Tukio la kihistoria kati ya viongozi wa Makanisa haya mawili!

Mama Angelica mwishoni mwa maisha yake, alijikita zaidi katika sala na tafakari; katika ukimya, huku akiishi na watawa wenzake. Mama Mary Angelica anatarajiwa kuzikwa kwenye Madhabahu Ekaristi Takatifu, huko Hanceville, Ijumaa tarehe 1 Aprili 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.