2016-03-28 14:26:00

Kristo Mfufuka ni tumaini la waja wake!


Wakristo sehemu mbali mbali za dunia wanaendelea kushangilia Siku kuu ya Pasaka, huku mioyo yao ikiwa imesheheni furaha ya Pasaka kwani Kristo amefufuka kweli kweli. Kipindi cha Kwaresima ilikuwa ni nafasi kwa waamini kutubu na kumwongokea Mungu hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baada ya maadhimisho ya Juma kuu, waamini bado wako mbele ya Kaburi tupu la Yesu, huku wakitafakari Fumbo la Ufufuko wa Bwana!

Tafakari hii imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu inayotumiwa wakati wa Kipindi cha Pasaka, Jumatatu, tarehe 28 Machi 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tukio ambalo limehudhuriwa na umati mkubwa wa waamini na wageni kutoka sehemu mbali mbali za dunia ambao kwa sasa wako mjini Roma kusherehekea Pasaka ya Bwana.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, nguvu ya maisha imekishinda kifo; huruma ya Mungu imeshinda dhambi, changamoto ya mwanga wa imani na matumaini kuambata mwelekeo huu mpya unaotambua kwamba, kweli Yesu Kristo amefufuka kwa wafu! Ukweli huu ukawa ni mwanzo wa mageuzi makubwa katika maisha ya Mitume wa Yesu, wakaanza mchakato mpya wa kumfuasa Mwalimu wao na baada ya kumpokea Roho Mtakatifu wakajitosa kimasomaso pasi na woga kile walichoshuhudia na kuona kwa macho yao wenyewe!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kutangaza na kushuhudia kwa nguvu kabisa kwamba, Kristo tumaini lao amefufuka kwa wafu! Mwaliko wa kuwa na mwelekeo mpya katika maisha, hata pale mambo yanapokwenda kinyume kabisa na matarajio yao! Hiki kinaweza kuwa ni kipindi cha giza, kuteleza na kuanguka tena dhambi.

Waamini wanapogusa kilindi cha umaskini na mapungufu yao ya maisha, Yesu anawakirimia tena nguvu ya kuweza kusimama, ikiwa kama waamini watamtumainia, neema yake itawaokoa! Yesu mteswa amefufuka, kielelezo na ushuhuda makini wa huruma ya Mungu iliyopo na inayoendelea kutenda kazi katika historia. Huu ndio ujumbe wa Pasaka unaoendelea kusikika tena na tena katika kipindi hiki cha Pasaka hadi wakati wa Siku kuu ya Pentekoste!

Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria alikuwa ni shuhuda wa matukio ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Alithubutu kusimama chini ya Msalaba, wala hakushindwa na machungu ya mateso ya Mwanaye mpendwa, kwani imani yake ilikuwa imara, ikamwezesha kuwa thabiti, huku moyo wake ukiendelea kuwaka moto wa matumaini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Bikira Maria ili awasaidie kupokea kwa ukamilifu tangazo la Pasaka juu ya Ufufuko wa Kristo, ili kuweza kuumwilisha katika uhalisia wa maisha. Bikira Maria awasaidie kuimarisha imani katika hija ya maisha, inayoangaziwa na mwanga wa Pasaka, ili iweze kuwa ni baraka na furaha kwa wengi, hususan kwa wale wanaoteseka kutokana na ubinafsi na hali ya kutoguswa na mahangaiko ya wengine!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.