2016-03-28 10:22:00

Kristo Mfufuka awape ujasiri na matumaini!


Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anasikitika kusema kwamba, mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea kwenye Uwanja wa Lahore Jumapili ya Pasaka, tarehe 27 Machi 2016 na kusababisha vifo vya watu 70 wasiokuwa na hatia na zaidi ya watu 340 kujeruhiwa vibaya yanachafua maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka. Bado vitendo vya chuki na uhasama vinaendelea kusababisha majanga kwa watu wasiokuwa na hatia!

Baba Mtakatifu Francisko baada ya kupewa taarifa hii, amesikitishwa na kwamba, anaendelea kusali kwa ajili ya kuwaombea wale walioguswa na shambulizi hili la kigaidi! Baba Mtakatifu yuko karibu na majeruhi, ili waweze kupona haraka na kurejea katika shughuli zao za kila siku! Inasikitisha kuona kwamba, Wakristo ambao ni wachache nchini Pakistan, bado ni walengwa wa vutendo vya kigaidi na misimamo mikali ya kidini. Mashambulizi haya yametikisha Pakistan katika ujumla wake!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Siku kuu ya Pasaka, licha ya mashambulizi ya kigaidi na umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia; Kanisa linaamini kwamba, Kristo Amefufuka kweli kweli na anaendelea kuwakirimia waja wake ujasiri na matumaini, mambo msingi katika ujenzi wa mshikamano na upendo na wale wote wanaoteseka kwa kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano, haki, amani na upatanisho wa kitaifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.