Baba Mtakatifu Francisko , akiongoza Ibada ya Mkesha wa Pasaka, katika homilía yake aliwaonya Wakristo kuitangaza furaha ya kweli ya Pasaka si kwa maneno lakini kwa vitendo ili kwamba Ukristo usionekana kama ni chama au shirika la Kimataifa lenye kuwa na wafuasi wengi na sheria teletele. Alisisita Wakristo ni lazima waonyeshe tumaini jema linalotafutwa na watu wengi. Akiongoza Ibada hiyo ya Mkesha wa Pasaka Papa alibatiza wakatukumeni 12 wakiwa ni raia wa Italia, Cameroon , Korea, India na China.
Katika homilía yake , Papa alitafakari kitendo cha Mtume Petro kukimbilia katika kaburi la Yesu baada ya kupewa habari na wanawake kwamba Yesu hayumo kaburini, akitoa ufafanuzi kwamba, Petro hana tena nafasi ya kuendelea kufunikwa na giza la huzuni , lakini aliruhusu mwanga wa Mungu kuingia moyoni mwake. Akili na moyo wa Petro mara viliguswa na habari kwamba Bwana wake hayumo kaburini. Petro ingawa hakuamini ushuhuda wa wanawake, hakubaki ameketi alipokuwa, hakubaki amejiinamia katika huzuni ya kifo cha mpendwa mwalimu wake, aliyemkana mara tatu, bali hima, aliinuka na kukimbilia kaburini. Papa amesema, hili linaonyesha mabadiliko ndani ya moyo wake . Huu ulikuwa ni mwanzo wa moyo wa Petro kufufuka kutoka mawazo ya kale. Moyo wake unapata wogofu mpya, uliofukuza giza la woga, huzuni na mashaka na badala yake kujawa na matumaini, akiruhusu mwanga wa Mungu kuingia moyoni mwake, na kubadilisha maisha yake.
Kama ilivyokuwa kwa Petro na wanawake, waliotoka mapema asubuhi kwenda kufanya tendo la huruma kuuhudumia mwili wa Yesu , wanawake waliokuwa wamechukua Marhamu na manukato kaburini, wanawake waliokuwa mwanzo wamejawa na hofu na kuinamisha vichwa vyao, kwa maneno ya malaika yaliyosema mnamtafuta aliye hai kati ya wafu, vivyo hivyo nasi hatupaswi kubaki tumejifungia ndani ya uchungu wetu wenyewe , lakini ni lazima kuiskiliza sauti ya Malaika anayevunja mihuri ya makaburi yetu ya kiroho na kutupa ujumbe kwamba Yesu amefufuka hayumo tena Kaburini . Ni muhimu kumruhusu Yesu Mfufuka aingie mioyoni mwetu., ili mwanga wake umulike katika changamoto nyingi zinazotukabili, na kuwa na utambuzi kwamba Yeye daima yu upande wetu na wala hatatutelekezi.
Papa aliendelea kusisitiza kwamba hatuwezi kugundua hali ya maisha yetu kwa kubaki tumejifungia katika dimbwi la huzuni, woga na mashaka kwa kuishi bila ya kuwa na matumaini. Tusiendelee kukaa ndani ya vifungo vyetu wenyewe, lakini tuivunje mihuri ya makaburi yetu na kutoka nje, ili Bwana apate kuingia katika maisha yetu. Ni lazima kuachana na hofu za nyuma , udhaifu wa nyuma na maporomoko ya nyuma na kumpa mkono Yesu anayetaka kutuokoa katika dhiki zetu.. Papa alieleza na kuhimiza kwamba, usiku huo ulikuwa ni usiku wa kulisongeza kando jiwe la dhambi, dhambi zinazotufnga ndani ya utumwa wa maisha. Aliendelea kumwomba Bwana, atuweke huru dhidi ya mitego ya kuwa Wakristo wasiokuwa na matumaini, kuishi kama vile Bwana hakufufuka, kama vile hayuko katikati ya matatizo ya maisha yetu.
Hata hivyo Baba Mtakatifu aliweka bayana kwamba, hii haina maana kwamba, hatutapambana na matatizo. Matatizo ya kidunia yataendelea kuwepo daima, ndiyo maana tunatakiwa kukesha macho, kuupokea mwanga huu wa usiku huo wa Pasaka , mwanga wa kipekee wa Bwana Mfufuka wenye kumlika katika matatizo yetu, ukitutaka tusiruhusu giza na hofu ya kudhibiti maisha yetu; lakini tuongeze matumaini yetu na furaha yetu kubwa kwamba, Bwana Mfufuka daima yu upande wetu na kamwe hatutelekezi.
Huu ndiyo msingi wa tumaini letu, si matumaini yenye mtizamo ya kisaikolojia au kutafuta ufahari wa kidunia lakini ni kuwa na matumaini ya maisha mazuri ya Kikristo, ambayo ni zawadi kutoka kwa Mungu. Zawadi yenye kutupa uhuru wa kweli wenye kufungua furaha zote za mioyo yetu kwake. Tumaini lisilo hadaa kwa sababu, humiminwa na Roho Mtakatifu mioyoni mwetu. Papa aliitaja Ibada hiyo ya Usiku kuwa ni adhimisho la tumaini hilo, adhimisho la ukweli huo, na wala hakuna kitu kinachoweza kulitenga na upendo wa Bwana kwa binadamu.
Kwa maelezo hayo , Papa alitoa wito akimtaka kila mtu, kutoka nje na kuutangaza Ujumbe huu wa kwa nia ya kuamsha na kufufua ari mpya katika matumaini kwa mioyo iliyozongwa na mzigo na huzuni na dhambi. Kwa wale wanaopambana na changamoto katika kupata maana ya maisha yenye matumiani baada ya maisha haya ya kidunia. Mkristo ni lazima kutangaza matumaini ya maisha yajayo ya mbinguni , kama watumishi wa matumaini hayo ya Upendo wa Kristo Mfufuka kwa kila binadamu, vinginevyo Ukriso unakuwa kama chama tu au shirika la kimataifa lenye wafuasi wa sheria nyingi nzuri, lakini wasiokuwa na matumaini kwa maisha ya baadaye .
Papa alitaja jinsi ya kuimarisha moyo katika tumaini hili, akisema ni kwa kukumbuka kazi za Mungu, uaminifu wa Mungu na historia ya upendo wake kwetu. Na muhimu kusoma Neno la Injili lenye kutukumbusha maneno yna matendo ya Bwana wetu Yesu Kristo. Vinginevyo alionya tutapoteza matumaini. Ni kukumbuka wema wake na maneno ya Yesu yenye kugusa na kuhuisha mioyo yetu. Haleluya Bwana Yesu amefufuka Haleluya!
All the contents on this site are copyrighted ©. |