2016-03-27 10:20:00

Idadi ya wahamiaji duniani imefikia watu millioni 244!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Pasaka kwa mwaka 2016 “Urbi et Orbi” anasema, Kristo Mfufuka anawatangazia walimwengu wote Injili ya uhai, kwa kuwakumbuka na kuwasaidia watu wanaotafuta maisha bora zaidi; hawa ni wakimbizi na wahamiaji; kati yao kuna watoto wanaokimbia vita, baa la njaa, umaskini na ukosefu wa haki msingi jamii. Kwa masikitiko makubwa, watu hawa wakiwa njiani kwenye hija ya matumaini wanakumbana na kifo; ukatili kiasi hata cha kushindwa kukubaliwa kuingia na kupewa msaada wanaohitaji.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Mkutano wa Kimataifa kuhusu Ubinadamu utatoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na utu wake, ili kuibua sera na mikakati inayoweza kuwasaidia na kuwalinda waathirika wa vita, dhuluma na nyanyaso za kidini. Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2015 kumekuwepo na wahamiaji zaidi ya millioni 244 duniani, kiasi ambacho ni ongezeko la asilimia 41% katika kipindi cha mwanzo wa karne hii.

Taarifa inaonesha kwamba, idadi kubwa ya wahamiaji ni wale wanaotoka Barani Asia, wengi wao wakiwa ni wale wanaotoka India, China, Bangaladesh na Pakistani. Bara la Ulaya pia linaonesha kwamba, watu wake pia wanatafuta ubora wa maisha sehemu nyingine za dunia, wengi wao ni wale wanaotoka Russia na Ukraine. Umoja wa Mataifa unaonesha kwamba, idadi ya wahamiaji wanawake duniani katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2015 imeshuka kwa asilimia 48.2%. Lakini kiwango hiki kwa Ulaya na Amerika kimeongezeka kwa asilimia 52%. Wengi wa wanawake hawa ni wale wanaofanya kazi za majumbani kwa ajili ya kutoa huduma kwa wazee wanaoendelea kuongeza kwa kasi kubwa Barani Ulaya na Amerika.

Umoja wa Mataifa unafafanua kwamba, umri wa wastani kwa wahamiaji hawa ni kati ya miaka 38 hadi 39, wahamiaji kutoka Barani Afrika wanaongoza kwa kuwa na umri mdogo zaidi, wastani wao ukiwa ni miaka 28 hadi 29. Idadi ya wakimbizi wenye umri mdogo chini ya miaka 20 ni millioni 37 hiki ni kiasi cha asilimia 15% ya idadi yote ya wajamiaji duniani!

Umoja wa Mataifa unakaza kusema, wahamiaji wamekuwa na mchango mkubwa katika mchakato wa ukuaji wa uchumi kwa nchi wahisani, hususan Barani Ulaya, ingawa wanakabiliwa na mazingira magumu ya maisha. Wakimbizi na wahamiaji wengi ni nguvu kazi, watu wanaoweza kutumiwa kikamilifu katika mchakato wa uzalishaji na utoaji wa huduma kwa jamii. Hata hivyo taarifa inaonesha kwamba, watu waliovuka umri wa miaka 65 ni millioni 30 sawa na asilimia 30% ya wahamiaji wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.