2016-03-26 10:28:00

Pasaka ya Bwana!


Leo tunaadhimisha kilele cha Ukristo wetu: Bwana wetu Yesu Kristo amefufuka, kweli kweli. Yu mzima na hayuko kaburini. Giza limetoweka na nuru imetuangaza, mauti imeshindwa yu mzima kweli. Ukuu wa sherehe hii unajionesha katika urefu wa adhimisho lake kwani sherehe hii huadhimishwa kwa muda wa siku hamsini ambazo hutanguliwa siku kuu tatu ambazo zinabeba maana ya fumbo zima la Pasaka yaani siku ya Ijumaa kuu ambayo huanzia Alhamisi kuu jioni kwa adhimisho la Karamu ya Bwana, Jumamosi kuu na Dominika ya Pasaka. Kanisa halichoki kutueleza maana ya siku kuu hii kwamba ni kutoka katika hali ya upotevu na kuingia katika hali ya uzima wa kimungu. Sisi tuliokufa katika dhambi zetu tumefufuka katika Kristo na tunaishi pamoja naye. Ishara ya ushindi huo ni Mshumaa wa Pasaka, Mwanga wa Kristo uondoao giza, ishara ya dhambi na mauti.

Ufufuko wa Kristo ni hakika. Hili ndilo linalotutia nguvu na kuyabeba yote aliyotufundisha kama ukweli ili nasi kujipatia uzima wa kimungu tulioupoteza kwa dhambi. Ushuhuda wa ufufuko wake unaelezwa wazi tena katika hali ya ujasiri kabisa na wafuasi wake wakiongozwa na mtume Petro kwamba: “Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika, si kwa watu wote, bali kwa mashahidi waliokuwa wamekwisha kuchaguliwa na Mungu, ndiyo sisi, tuliokula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu”. Matendo hayo ya kula na kunywa pamoja naye yana lengo la kukazia kwamba aliyefufuka ni Yeye alikufa msalabani, Kristo mwana wa Mungu, Mungu kweli na mtu kweli. Si mzimu bali Yeye yuleyule.

Somo la Injili linatuambia kwamba Petro na yule mwanafunzi aliyependwa na Bwana walifika kaburini kuhakikisha juu ya habari waliyoletewa na Mariamu Magdalena kwamba “wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walokimweka”. Sehemu hii ya Injili inatueleza kwamba waliona na kuamini juu ya ukweli huu kwamba Bwana hayupo kaburini. Ila ukweli wa kwamba amefufuka unadhihirika zaidi katika matendo yanayofuata baada ya kutokuonekana kaburini, yaani, kujitokeza kati ya wanafunzi wake na kula na kunywa pamoja nao. Sehemu ya Injili hiyo inayoendelea baada ya hili tunalosikia katika dominika hii inaonesha jinsi Kristo mfufuka alivyowatokea wafuasi wake.

Kwanza kabisa anamtokea Mariamu Magdalena ambaye anakwenda kushuhudia kwa wafuasi wake kwamba “Nimemwona Bwana” (Yoh 20:11 – 18). Pia anawatokea wanafunzi wake mara mbili wakiwa wamejifungia tunaambiwa kwa hofu ya wayahudi na kuwaonesha majeraha yake uthibitisho wa mwili wake Yeye aliyesulubiwa msalabani kuwa ni ule ule wa Yeye aliye fufuka. (Rej. Yoh 20:19 – 29). Zaidi ya hapo aliwatokea katika shughuli za uvuvi na hapo alikula na kunywa pamoja nao (Rej Yoh 21:1 – 14).

Hivyo, Neno la Mungu linatupatia uthibitisho kwamba yu mzima. Yule ambaye walidhani kwamba ameshindwa yu mzima kwa sababu ufalme wake si wa dunia hii na makusudi yake ni kuleta mwanga katika giza la ulimwengu huu. Giza linashindwa na sasa nuru inatawala na huu ndiyo wito mkubwa wa maisha ya kikristo, yaani kuwa mashuhuda wa maisha ya mwanga. Mada kuu inayojikita katika sherehe hii kubwa ya imani yetu ya kikristo ni upya wa maisha unaochipuka katika Kristo mfufuka. Katika somo la pili mtume Paulo anatuambia: “Pasaka wetu amekwisha kutolewa sadaka, yaani Kristo; basi na tuifanye karamu si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli”. Huu ni mwaliko wa upya wa maisha, maisha ya kipasaka,  maisha ambayo yanashuhudia zaidi kwamba giza limekwisha kutoweka na nuru inatuangaza, maisha ambayo yanathibitisha kwamba kweli Kristo yu mzima.

Katika Misa ya Kesha la Pasaka tunaambiwa kwamba: “Kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu? Hayupo hapa, amefufuka”. Ukristo unatualika kuishi maisha ya uhai tele, maisha yenye matumaini, maisha ambayo daima yanaufunua utukufu wa Mungu na kuunganika naye katika mpango wake wa wokovu. Mtume Paulo anatuambia kwamba “basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi”. Ni mwaliko wa kuishi maisha ya ushuhuda kwa ulimwengu.

Ushuhuda wetu kwa nafasi ya kwanza utamfanya Kristo aendelee kuwa hai katika ulimwengu wa leo. Ushuhuda huu si jambo jingine bali ni kuishi ukristo wetu, yaani, kuidhihirisha hadhi yetu tuliyorudishiwa na Kristo ambayo tuliipoteza kwa dhambi. Hii nichangamoto kwetu sisi wabatizwa na hasa pale maisha yetu yanapoonekana kusawazishwa na uovu wa dunia hii. Mkristo anaposhindwa kuwa sababu ya mshangao kwa jamii na kufanya maisha yaonekane “business as usual” ni usaliti kwa maisha ya ufufuko. Imani tunayokiri kwamba Kristo amefufuka inapaswa kwenda sawia na imani tunayoishi. Tunapoendelea kushuhudia na hata kushiriki katika uovu mbalimbali wa kijamii humaanisha kwamba bado tunamtafuta aliye hai makaburini.

Kwa nafasi ya pili ushuhuda huo unajionesha katika maisha yetu ya kindugu. Maisha haya kwa namna ya pekee huchagizwa na Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ambayo inaendelea kuweka hai sadaka ya Kristo aliyoitoa msalabani kwa ajili yetu. Sakramenti hii inatufanya tuwe sawa na hicho tunachokipokea, yaani, Yeye Kristo mfufuka. Uwepo wa Sakramenti hii unaimarisha umoja na undugu kati yetu wakristo na zaidi unatupatia uwezo wa kufunguka na kutoka nje, yaani, kuwa kuwa vyombo vya kuieneza huruma ya Mungu hasa kwa wale walidharaulika na walio pembezoni. Upendo wetu wa kipasaka ni muhimu kwao na pia huwawezesha kuionja faraja ya Mungu ambayo inakamilishwa katika jamii ya mwanadamu kwa Fumbo hili la Pasaka.

Kwa nafasi ya tatu ushuhuda wa maisha ya kipasaka uisaidie jamii ya waamini kuwa chachu ya mabadiliko kwa maisha ya vijana wetu wa leo. Ushuhuda huu ni muhimu sana kwao kipindi hiki pengine kuliko wakati mwingine wowote. Fumbo la pasaka ni alama ya ushindi wa Mungu dhidi ya upepo wa kidunia. Dunia hii inawavutia vijana wetu katika kuona furaha katika vitu vya kushikika na vyenye kupita tu. Tumaini lao wengi limewekwa katika mali, vyeo, starehe na anasa za kidunia. Pengine imani yetu imeshindwa kuwa na ushawishi kwao wa kuoinja furaha ya kweli ipatikanayo kutoka kwa Mungu. Hivyo tuelekeze ushuhuda wetu pia kwa hawa wapendwa wetu ambao ni nguzo na tegemeo kwa Kanisa na jamii nzima ya mwanadamu.

Hivyo ninakualika katika dominika hii ya Pasaka kufufuka pamoja na Kristo na neema ya ufufuko wake Kristo ikuongoze katika kutafuta kweli na kuiishi hiyo kweli kwa maisha ya ushuhuda. Ukristo wetu uwe ni wa kimatendo zaidi kusudi upate kuwavuta wengi na kuwaingiza katika ukweli ambao ndiyo unaoustawisha ufalme wa Mungu hapa duniani. Bwana amefufuka kweli kweli, Aleluya! Utukufu na ukuu una Yeye, Aleluya!

Tafakari hii imeletwa kwako nami Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.