2016-03-26 08:45:00

Huduma makini kwa Familia ya Mungu Roma!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Ibada ya kubariki Mafuta Matakatifu yatakayotumika kwenye maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali, Alhamisi kuu, tarehe 24 Machi 2016 alipata chakula cha mchana pamoja na baadhi ya Maparoko kutoka Jimbo kuu la Roma. Wakati wa chakula cha mchana, Baba Mtakatifu na wageni wake waliweza kuzungumza masuala mbali mbali ya maisha, shughuli za kichungaji na changamoto zake!

Lakini mkazo mkubwa ulikuwa ni huduma makini kwa Watu wa Mungu, hususan maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwani hawa ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu, hususan wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu! Baba Mtakatifu amewasikiliza kila mmoja wao, akionesha shauku ya kutaka kujifunza mapya kutoka kwa mapadre wake wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa.

Maparoko wamemwelezea Baba Mtakatifu Francisko jinsi ambavyo wanajitahidi kumwilisha huduma ya Neno, Sakramenti na matendo ya huruma miongoni mwa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma. Hii ni familia ambayo inafanya hija ya kuendelea kugundua utajiri wa Injili unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha adili na matakatifu; kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema, mambo ambayo yanapaswa kutekelezwa na familia katika mchakato wa utekelezaji wa wito na dhamana yake ndani ya Kanisa na kwa jamii katika ujumla wake.

Mapadre hawa wamekiri kwamba, yataka moyo kweli kweli kuwa Padre na mhudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa mjini Roma! Hili ni Jiji lenye changamoto na karaha zake; mahali panapohitaji sadaka na majitoleo binafsi yanayojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo makini cha imani tendaji! Inafurahisha kuona kwamba, waamini walei wako mstari wa mbele katika kulitegemeza Kanisa kwa hali na mali pamoja na ushiriki wao mkamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Roma ni mahali ambapo panapaswa pia kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene.

Utume na maisha ya Papa Francisko ni changamoto kubwa na endelevu inayopania kuleta chachu ya mageuzi katika maisha na utume wa Kanisa. Pengine ni mapema mno kuweza kuona matunda ya mwelekeo huu, lakini mwenye macho na masikio, anaweza kujionea mwenyewe! Kanisa linapaswa kuwa ni shuhuda na chombo cha upendo na huruma ya Mungu kwa kuwasaidia waamini wanaoogelea katika shida mbali mbali; utume kwa vijana ili kuwapatia dira na mwelekeo mpya wa maisha; familia kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.