2016-03-25 09:56:00

Papa Francisko awaosha miguu wakimbizi!


Alhamisi Kuu majira ya Jioni , Baba Mtakatifu Francisko aliongoza Ibada ya Misa Takatifu,akiwa katika Kituo cha CARA ,  cha Castel Nouvo di Porto, nje kidogo ya jiji la Roma , kituo chenye kutoa makazi ya muda mfupi kwa wakimbizi karibia 900,  wanaotafuta hifadhi za kisiasa nchini Italia kutoka nchi mbalimbali .  Wakati wa Ibada ya Misa,  Papa Francisko aliosha miguu ya wahamiaji 11 na mhudumu mmoja wa kujitolea.  Wahamiaji hayo walikuwa ni mchanganyiko wa imani mbalimbali , watu wanne wakiwa  vijana Katoliki kutoka Nigeria, wanawake watatu Wakoptic kutoka Eritrea, Waislamu watatu na Mhindu mmoja kutoka India.

Wakati wa hotuba yake, Papa alionyesha kufurahia hali halisi yamchanganyiko huo akisema ni  ishara ya kupendeza ya watu wa dini na tamaduni tofauti kukaa  pamoja  kwa amani, kama watoto wa baba mmoja tu,  ikiwa  kinyume na ishara ya mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika siku ya  Jumanne huko Brussels.  Papa Francisko alirudia kukemea kwa nguvu wale wote wenye kupanda mbegu ya uchochezi wenye kutenganisha watu  kupitia njia mbalimbali,  kama ilivyokuwa kwa Yuda Iskariote - migawanyiko kutokana na utafutaji wa wa faida za kibiashara, biashara ya silaha na  zana zinazosababisha umwangaji wa damu .

Aidha Baba Mtakatifu  alizungumzia nguvu ya mawasiliano  katika ujenzi wa udugu, ushirikiano  mapatano na amani miongoni mwa watu wa dini tofauti na mila na tamaduni mbalimbali, watu wenye kuwa na hamu ya kweli ya kuishi kwa amani na kutatua changamoto zinazojitokeza , kwa moyo wa udugu wenye kushuhudiwa kimatendo, katika dunia ya leo  inayohitaji ishara kama hizo.

Papa alieleza  hayo, akionyesha kujali jinsi binadamu anayotaka kuona ishara kuliko kuona na au kusikia maneno matupu. Alirejea Neno la Mungu lililosomwa akisema, kuna ishara  mbili: Yesu anatufundisha kuhudumia wengine, kama alivyofanya kuwaosha miguu mitume wake. Hii ni ishara ya kuhudumia kwa upendo mkuu bila kujibakiza. Na pia katika  masomo hayo kuna ishara ya pili ambayo ni usaliti. Kitendo kilichofanywa na Yuda Iskarioti kumuuza Yesu kwa maadui wake , wasiopenda amani,  kwa vipanda 30 vya fedha. Hii ni ishara inayoonyesha jinsi tamaa ya mtu anayetaka kupata faida binafsi asivyo jali kuharibu maisha ya mwingine. , Yuda alimsaliti Yesu kwa maadui zake kwa vipande 30 vya fedha.

Papa alianisha utendaji huo na hali halisi za wakati huu akisema , wakiwa mahali hapo, wanashuhudia ishara hizi mbili: Ishara ya kwanza, ikiwa ni kuhudumiana kama  jinsi walivyokusanyika hapo kwa pamoja wakiwa waaamini wa dini na tamaduni mbalimbali ,  Waislamu, Wahindu, Wakatoliki, Wakristo, kama  watoto wa Mungu wanaotaka kuishi kwa amani, kuishi kwa pamoja katika hali hiyo mchanganyiko.  Na pia bado wanakumbukumbu ishara ya pili , iliyoonekana  siku tatu zilizopita, tendo la vita, na uharibifu katika mji wa Brussles , iliyofanywa na  watu wasiotaka kuishi kwa amani. Kama ilivyokuwa kwa Yuda Iskariote nyuma yake kuwa na watu wengine, na ndivyo ilivyokuwa  ishara ya vita nyuma yake kuna watu wengine , wanaotoa fedha kwa ajili ya kusababisha vurugu hizo. Wafanyabiashara wanaotafuta faida kwa kumwaga damu ya wengine, wanaotaka vita na si udugu .

Papa alieleza na  kufafanua tukio la yeye kufanya kama Yesu, kuosha miguu ya watu kumi na wawili, kwamba alilenga  kuonyesha  ishara ya udugu, ishara ya umoja, licha ya  tofauti za tamaduni mbalimbali za kidini, inawezekana wote kujiona kama ndugu wanaopenda kuishi kwa amani. Papa alieleza na kuomba, ili kwamba  maisha ya kila mmoja yaweza kuonyesha ishara hii ya kuhudumu kwa upendo , licha ya uwepo wa misalaba na matukio mengi ya  kuhuzunisha. Alimwomba Bwana ili kwamba udugu huu ulioonekana katika kituo hicho cha CARA uweze kueneo pote duniani , ili kusiwe na haja ya kumuuza ndugu katika njia za mauaji kwa  vipande 30 vya fedha, ila daima iwe  kujenga udugu na wema. 

Baada ya Ibada ya Misa, Papa alitoka nje na kusalimiana ana kwa ana na wakimbizi wote wa kituo hizo kama ishara ya umoja na mshikamano wa kidugu, changamoto inayopaswa kufanyiwa katika na wengi ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati! 








All the contents on this site are copyrighted ©.