2016-03-25 07:53:00

Ekaristi Takatifu inalijenga Kanisa!


Yesu Kristo ndiye aneyelijenga Kanisa kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu yake Azizi, changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanaliadhimisha Fumbo hili kielelezo cha huruma na upendo wa Kristo kwa waja wake. Fumbo la Ekaristi Takatifu liwe ni utambulisho na kielelezo cha wafuasi wa Kristo! Haya ni maneno yaliyotolewa na Padre Andrzej Majewski, Mkurugenzi wa Vipindi, Radio Vatican wakati wa Ibada ya Misa Takatifu, Alhamisi kuu, Kanisa lilipokuwa linakumbuka Siku ile Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu na Amri ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini!

Katika mahubiri yake, Padre Jean-Pierre Yammine Talal kutoka Idhaa ya Kiarabu ya Radio Vatican alisema kwamba, Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Yesu aliweka Sakramenti ya Daraja takatifu na Ekaristi Takatifu; Mwili na Damu yake Azizi, uliotolewa sadaka pale Msalabani, sadaka inayoendelezwa kila wakati Kanisa linapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hii ni sadaka ambayo ni chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa.

Alhamisi kuu, Yesu aliwaosha miguu mitume wake, huduma iliyokuwa inatolewa na watumwa enzi hizo, lakini akaipatia maana mpya, yaani hii ni huduma ya upendo inayomwajibisha mwamini. Huu ndio utamaduni wa Kikristo wa kuhudumia unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo mwenyewe! Leo hii, Yesu anaendelea kuosha roho za waja wake kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho; upendo na huduma makini, mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa huduma ya upendo inayomwilishwa katika unyenyekevu wa maisha.

Ubora wa huduma unapimwa na changamoto inayobubujika katika upendo na kwamba, Kristo mwenyewe ndiye kielelezo cha utoaji wa huduma makini. Waamini wanapofanya kumbu kumbu ya kuanzishwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu anasema Padre Talal wanaalikwa kuendeleza dhamana na wajibu waliojitwalia wakati wa Sakramenti ya Ubatizo, wa kutoka katika ubinafsi wao, tayari kujitosa kimasomaso kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha kwa watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Wakristo wawe na ujasiri wa kuendeleza mchakato wa Sadaka ya Kristo Msalabani, kwa kuwashirikisha jirani zao: urafiki, huduma na uwepo wao; kwa majitoleo na sadaka yao; kwa taaluma na vipaji ambavyo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu. Kwa kumuiga Kristo kwa njia ya huduma makini, watu wataweza kutambua upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake! Waamini wawe tayari kumuiga Kristo aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya ndugu zake, ili waweze kuwa na uzima wa milele.

Kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Kristo anajenga Jumuiya ya waamini wanageuka na kuwa ni sehemu ya Fumbo la mwili wake, yaani Kanisa, linaloendelea kukua na kupanuka! Hii ndiyo Pasaka ya Bwana, Pasaka ambayo Kanisa linajiandaa kuiadhimisha, baada ya mateso na kifo cha Kristo, ili kuwafunulia walimwengu huruma na upendo wa Baba wa milele!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.