2016-03-24 10:14:00

Utufanye tuwe vyombo vya amani!


Viongozi mbali mbali wa Makanisa wameonesha kuguswa na kusikitishwa sana na mauaji ya kigaidi yaliyofanyika huko Ubelgiji na kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Wanamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwajalia kuwa kweli ni vyombo vya haki, amani, huruma na mapendo katika ulimwengu ambao umesheheni vita, ghasia, chuki, ubinafsi na hali ya kutaka kulipizana kisasi. Viongozi wa Makanisa wanapenda kuonesha uwepo wao wa karibu na wote walioguswa na vitendo hivi vya kigaidi huko Ubelgiji.

Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kupinga vitendo vyote vya kigaidi vinavyotaka kupandikiza mbegu ya chuki na uhasama kwa kujenga kuta zinazowatengnanisha watu; kuta ambazo zinapaswa kubomolewa, ili kujenga na kudumisha msingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu.

Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima anakaza kusema, vitendo vya kigaidi vinalenga kuleta mtafaruku kati ya watu na hivyo kubomoa msingi wa mafungamano na mshikamano wa kijamii. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuonesha upendo na mshikamano wa dhati, dhidi ya chuki na uhasama unaopandikizwa na magaidi sehemu mbali mbali za dunia. Kiongozi huyu anaiomba Serikali ya Ubelgiji kufikisha salam zake za rambi rambi kwa watu walioguswa na maafa haya ndani na nje ya Ubelgiji.

Kwa upande wake, Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema, wanesitikishwa sana na mauaji ya zaidi ya watu 30 na wengine zaidi ya 200 kujeruhiwa vibaya kutokana na mashambulizi ya kigaidi huko Brussels, Ubelgiji, Makao makuu ya Umoja wa Ulaya na Makao makuu ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Hivi ni vitendo vya kinyama vinavyohatarisha maisha ya watu Barani Ulaya! Wananchi Barani Ulaya washinde kishawishi cha chuki na hali ya kutaka kulipizana kisasi na badala yake wajenge na kudumisha moyo wa upendo na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maishao Barani Ulaya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.