2016-03-23 08:05:00

Alhamisi kuu: Papa Francisko kuwaosha miguu wahamiaji 12 kutoka Afrika!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Alhamisi kuu jioni, maarufu kama Karamu ya Mwisho, Siku ile Yesu alipoweka Sakramenti ya Daraja Takatifu pamoja Ekaristi Takatifu na kuwaosha mitume wake miguu, kielelezo cha huduma ya upendo inayodhihirisha huruma ya Mungu kwa mwanadamu, Baba Mtakatifu Francisko, majira ya saa 11: 00 jioni kwa saa za Ulaya, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kituo cha wahamiaji wanaomba hifadhi ya kisiasa nchini Italia na kuwaosha miguu wahamiaji kumi na mmoja na mfanyakazi mmoja wa CARA wakati wa Ibada hiyo!

Kituo hiki kijulikanacho kama CARA, yaani “Centro Accoglienza dei Richiedenti Asilo” kilichopo Castelnuovo di Porto, kipo nje kidogo ya mji wa Roma. Kituo hiki kwa sasa kinatoa hifadhi kwa wahamiaji 900 wengi wao wakiwa ni wale wanaotoka Barani Afrika. Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji mpya anasema, Ibada hii ya Misa Takatifu pamoja na kitendo cha Baba Mtakatifu Francisko kuwaosha miguu wahamiaji hawa ni changamoto ya kutoa huduma ya upendo sanjari na kuguswa na mahangaiko yao, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Mama Kanisa anapenda kutoa mwaliko kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia kuhakikisha kwamba, inawashughulikia na kuwahudumia maskini na wanyonge ndani ya jamii, ili kuwarudishia tena utu na heshima yao kama binadamu, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kukombolewa kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu. Hawa ni watu wanaokimbia kutoka katika vita, dhuluma, nyanyaso, umaskini na hali ngumu ya maisha! Ni umati wa watu unaotafuta usalama na hifadhi ya maisha, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha upendo na mshikamano kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji, ili kweli waweze kujisikia kuwa wako salama.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza Wakristo pamoja na taasisi mbali mbali za Kikristo kuonesha ukarimu kwa kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha Barani Ulaya, ili kuonesha umoja na mshikamano na wakimbizi pamoja na wahamiaji hawa ambao kwa sasa wamechoka na kujikatia tamaa. Kuna familia na taasisi ambazo zimeitikia wito huu wa Baba Mtakatifu Francisko na sasa zinatoa hifadhi kwa familia mbali mbali za wakimbizi. Hii ni changamoto kwa waamini kumwilisha ndani mwao huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, wakati huu Kanisa linapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba, Yesu Kristo kwa kuwaosha mitume wake miguu, amewafunulia binadamu utendaji wa Mungu katika maisha ya mwanadamu, kwa kutoa amri mpya ya upendo, ili kupendana wao kwa wao kama Kristo alivyowapenda pia. Ikumbukwe kwamba, upendo ni amri inayomwilishwa katika huduma makini inayojikita katika unyenyekevu, ukimya na sadaka sanjari na kushirikishana raslimali na mali ya dunia hii, ili kila mtu aweze kupata walau mahitaji yake msingi hapa duniani. Hiki ni kielelezo cha utu wema. Maadhimisho ya Juma kuu iwe ni fursa kwa waamini kujiandaa kikamilifu katika mchakato wa kumwilisha huruma na upendo wa Mungu unaojifunua kwa njia ya Fumbo la Pasaka yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Iwe ni Pasaka ya mshikamano na wale wote wanaoteseka kutokana na vita na majanga mbali mbali ya maisha. Iwe ni fursa ya kukazia umuhimu wa kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu. Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwaosha wahamiaji miguu, anawaalika watu kuwaheshimu na kuwathamini hata katika mateso na mahangaiko yao ya maisha anasema Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.