2016-03-22 08:03:00

Mungu ni mwenye huruma!


Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote. Huu ni utangulizi wa tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka magofu ya Colosseo mjini Roma, Ijumaa kuu tarehe 25 Machi 2016, wakati Mama Kanisa anapotafakari mateso na kifo cha Kristo Msalabani, chemchemi ya huruma ya Mungu, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya huruma ya Mungu! Itakumbukwa kwamba, tafakari hii imeandaliwa na Kardinali Gualtiero Basseti na maadhimisho haya yataongozwa na Baba Mtakatifu Francisko.

Mungu ni mwenye huruma ndiyo kauli mbiu ya tafakari ya Njia ya Msalaba kuzungumza magofu ya Colosseo ambayo ina vituo kumi na vinne kadiri ya Mapokeo ya Kanisa. Ni tafakari inayoonesha huruma ya Mungu katika hija ya maisha ya mwanadamu; Mungu anayefariji na kwamba, huruma ni chemchemi ya neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa watu wanaoteseka kutokana na majanga mbali mbali ya maisha; watu wanaonyanyaswa na kudhulumiwa utu na heshima yao kama binadamu. Ni mwaliko wa kuchunguza dhamiri, ili kutambua uwepo na madhara ya dhambi katika maisha ya mwanadamu, tayari kuambata huruma na upendo wa Mungu.

Kardinali Basseti anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kuinua macho yao ili kuutaza Uso wa Kristo mwenye huruma, ili kuonja tena upendo wake wa milele; kwa kusamehewa dhambi, tayari kuanza njia ya utakatifu wa maisha, kwa kukumbatia Msalaba kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu! Yesu Kristo ni chemchemi ya maisha ya uzima wa milele. Hii ni tafakari ambayo inagusa mateso na mahangaiko ya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.

Kuna Wakristo wanaoendelea kuteswa na kudhulumiwa sehemu mbali mbali za dunia; kuna familia zinazoogelea katika shida na mahangaiko makubwa: kiroho na kimwili. Njia ya Msalaba kuelekea Golgotha ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma ya Mungu kwa binadamu. Tafakari hii ya Njia ya Msalaba wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu inapenda kuwasindikiza waamini kutambua na kuonja huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika “Kashfa ya Msalaba”.

Mwili wa Yesu aliojaa damu tupu na madonda unamwonesha mwanadamu njia ya haki ya Mungu inayogeuza mateso na mahangaiko ya ndani kuwa ni mwanga wa Ufufuko. Lakini kama ilivyokuwa kwa Pilato aliyeogopa kupoteza umaarufu na usalama wake; kuna watu ambao pia wanaogopa kuambata Ukweli wa Mungu; kuna watu wanaendekeza sera za ubaguzi na utengano wa kijamii; kuna watu wanaowagopa wageni na wahamiaji kutokana na ubinafsi; lakini ikumbukwe kwamba, wote hawa wanaonesha Uso wa Kristo!

Njia ya Msalaba inatoa nafasi ya kutafakari mateso na mahangaiko ya Yesu anayeanguka chini ya Msalaba mara tatu kwa kuelemewa na uzito wa dhambi za binadamu. Wakati mwingine anasema Kardinali Basseti mateso na mahangaiko ya mwanadamu hayapati maana kamili, hapa ni mwaliko wa kutambua ile maana ya uhuru na nguvu ya maisha ya kiroho inayobubujika katika mateso na mahangaiko ya binadamu. Kuna watu wameanguka na kukwazika kutokana na ufunuo wa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai.

Hapa Kanisa linawakumbuka Wayahudi waliouwawa kwenye kambi za mateso; Wakristo wanaoendelea kuteswa, kunyanyaswa na kuuwawa kikatili kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kanisa linawakumbuka na kuwaombea watu wanaodhulumiwa kwa sababu mbali mbali! Katika Njia hii ya Msalaba, Yesu anakutana na Mama yake uso wa kwa uso; taswira inayotawala ni ile ya familia, chemchemi ya maisha ya binadamu, nguvu msingi ya mahusiano ya kibinadamu. Ujasiri wa Veronika kupangusa uso wa Yesu unashuhudia nguvu ya upendo katika sadaka na majitoleo ya watu.

Yesu anapoanguka mara ya pili, anawakumbusha waamini kwamba, wasipokuwa makini, wanaweza kuanguka mara kwa mara dhambini na kwamba, hapa wanahitaji nguvu na neema ya Kristo kuweza kusimama na kusonga mbele, hakuna mtu anayeweza kujiokoa mwenyewe! Kuna familia zinazoogelea katika shida na mahangaiko ya maisha ya kiroho na kimwili: kwa kukosa fursa za ajira; kuna umati mkubwa wa vijana ambao hawana matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi kutokana na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo katika maisha.

Kanisa linapenda kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwainua tena wale walioanguka kutokana na udhaifu wa kibinadamu kwa ndoa zao kusambaratika; kwa majanga na maafa mbali mbali au kwa kukata na kujikatia tamaa, ili wote hawa waweze kuguswa na huruma ya Mungu, tayari kuwa na ujasiri wa kusonga mbele kwa imani na matumaini!

Yesu anavuliwa nguo! Ni kitendo cha unyanyasaji usiokuwa na kifani, unaolikumbusha Kanisa watoto walionyanyaswa na kudhulumiwa kijinsia, jinsi  ambavyo utu na undani wao wa maisha ulivyochafuliwa na watu waliofilisika kimaadili. Lakini kwa njia ya Msalaba, Yesu anaonesha ile nguvu ya Kimungu ndani mwake na kwamba, kwa njia ya unyenyekevu, akakubali mateso na kifo cha aibu Msalabani; kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Huu ni upendo unaogeuzwa kuwa sadaka ambayo Kristo anaikubali na kuiambata kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti!

Akiwa Msalabani, kuna hata wale wanyang’anyi wawili waliokuwa wanateseka pamoja na Yesu, mmoja wao akathubutu kumdhihaki Yesu, ili ashuke Msalabani na kuwaokoa hata wao pia! Hiki ni kishawishi cha kukimbia Fumbo la Msalaba katika maisha ya mwanadamu! Hapa mantiki ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine unajionesha wazi wazi! Yule mwizi wa pili anakubali mapenzi ya Mungu na kumgeukia Kristo Yesu, ili aweze kumshirikisha tone la utamaduni wa upendo na msamaha! Yesu anapoinisha kichwa na kufa Msalabani, anaadhimisha kilele cha Fumbo la Huruma ya Mungu kwa binadamu; ushuhuda wa imani thabiti uliooneshwa na mashuhuda wa imani pamoja na wafiadini wa nyakati mbali mbali katika historia, maisha na utume wa Kanisa.

Yesu Kristo anapokamilisha hija ya maisha yake hapa duniani, anashuhudia kwa namna ya pekee kabisa ile nguvu ya imani, changamoto kwa waamini kuonesha upendo na mshikamano unaojikita katika ukarimu kwa maskini kama alivyofanya Yusufu wa Arimathaya aliyeomba ruhusa ili aweze kuuzika mwili wa Yesu kwa heshima! Kaburi la Yesu linafungwa kwa mawe! Lakini ikumbukwe kwamba, kifo hakina sauti ya mwisho katika maisha ya Kristo Yesu! Katika hali ya giza na ukimya pale kaburini, Mwenyezi Mungu bado anaendelea na kazi, anataka kumwonesha mwanadamu huruma na upendo wake usiokuwa na kifani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.