2016-03-22 10:08:00

Kenya simameni kidete kulinda Injili ya uhai!


Familia ya Mungu nchini Kenya inahimizwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, inasimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya uhai inayojikita katika kuthamini maisha ya binadamu, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu! Uhai ni sehemu ya haki msingi za binadamu na hakuna mtu awaye yote anayeruhusiwa kuichezea zawadi hii kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Askofu Salesius Mugambi, Mwenyekiti wa Programmu ya Familia, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya wakati wa uzinduzi wa Sala kwa ajili ya matembezi ya kuenzi Injili ya uhai, Jimbo kuu la Nairobi, Kenya. Askofu Mugambi anakaza kusema, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kulindwa, kutunzwa na kudumishwa na wote dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini!

Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai, kinyume kabisa na mwelekeo wa watu wengi katika jamii wanaoendelea kushinikizwa kukumbatia utamaduni wa kifo kwa madai kwamba, utoaji mimba ni haki ya mwanamke, kinyume kabisa na mapenzi ya Mungu. Wananchi wanapaswa kusimama kidete kupinga sera zinazokumbatia utamaduni wa kifo.

Wazazi na walezi wawe mstari wa mbele kushuhudia tunu msingi za maisha ya kifamilia, utu wema tayari kukumbatia Injili ya familia dhidi ya utamaduni wa kifo! Wazazi wawasaidie watoto na vijana wao kuwa na malezi bora yatakayowawajibisha kama raia wema na waamini wachamungu.  Katika matembezi haya ya kuunga mkono Injili ya uhai, Askofu na kundi kubwa la waamini walitembea kwenye mitaa na viunga vya Jiji la Nairobi kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Waandamanaji hawa wamelaani na kusikitishwa na vitendo vya utoaji mimba na kifo laini vinavyozidi kuongezeka kila kukicha; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; utumwa mamboleo; rushwa na ufisadi mambo ambayo yanadhalilisha utu, heshima na mafungamano ya kijamii. Maandamano haya yamehudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Nairobi, Kenya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa Rose Achiego, Radio Waumini, Kenya.  

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.