2016-03-21 07:38:00

Kumbu kumbu ya mashuhuda wa imani!


Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, Jumanne, tarehe 22 Machi 2016 majira ya jioni, ataongoza Sala ya mkesha kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea mashuhuda wa imani wanaoendelea kuyamimina maisha yao kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hawa ni wale wanaoteswa na kunyanyaswa; wanaotengwa na kubaguliwa; wanaonyimwa uhuru wao wa kuabudu kiasi hata kuuwawa kikatili, sehemu mbali mbali za dunia!

Ibada hii ya mkesha itaadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria wa Trastevere lililoko mjini Roma kuanzia saa 12: 30 jioni. Kardinali Stella katika tafakari yake kipindi hiki Kanisa linapokumbuka mateso, kifo na ufufuko wa Kristo anasema, Yesu Kristo ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu; anatambua maana ya mateso na upendo unaookoa, changamoto kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa upendo wake wa dhati kwa binadamu!

Yesu ni kielelezo makini cha huruma na upendo wa Mungu kwa jirani na kwa Muumba mwenyewe, asili na chemchemi ya wema na huruma yote! Waamini wanapaswa kutambua kwamba, hakuna Pasaka isiyokuwa na Kwaresima! Hapa waamini wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda wa wema, utakatifu na huruma ya Mungu kwa jirani zao. Kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu kwa kufuata mkumbo wa dunia.

Waamini katika mapambazuko ya millenia ya tatu ya Ukristo wanahamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha, kwa kuonesha na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, sababu na chanzo cha furaha yao ya ndani, hata kama wanazingirwa na magumu ya maisha. Juma kuu kiwe ni pindi cha kutafakari kwa kina na mapana Uso wa huruma ya Mungu unaojionesha katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo!

Kwa njia hii, waamini wataweza kuwa na ujasiri wa kusonga mbele pale wanapokabiliwa na mateso, dhuluma na nyanyaso katika maisha yao. Daima watambue kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa rehema na mapendo, anafariji, anaponya na kumkomboa mwanadamu anayekimbilia katika huruma na upendo wake. Hapa waamini wanapaswa pia kuguswa na shida pamoja na mahangaiko ya jirani zao sehemu mbali mbali za dunia, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa nyakati hizi.

Kardinali Stella anakaza kusema, hii ndiyo maana ya Mungu kuwa na huruma, ambayo inamwilishwa pia katika uhalisia wa maisha ya watu! Maadhimisho ya Juma kuu wakati huu wa maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu ni muda muafaka wa kutubu na kumwongokea Mungu; ni kipindi cha kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Hata katika udhaifu na mapungufu ya kibinadamu, waamini wajitahidi kutengeneza mwanya utakaopenyeza huruma ya Mungu katika maisha yao na yale ya jirani zao! Mwamini atambue kwamba, anapendwa na kusamehewa dhambi zake na Mwenyezi Mungu, ikiwa kama atajitahidi kupiga moyo konde na kukimbilia kwenye kiti cha huruma ya Mungu. Kwa njia hii, mwamini aliyetubu na kumwongokea Mungu, ataweza kujivika fadhila ya msamaha, tayari kuwasamehe wale waliomkosea. Changamoto hii kwa namna ya pekee, inawagusa Mapadre ambao kimsingi ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, dhamana wanayoitekeleza kwa njia ya Sakramenti ya Daraja Takatifu, Ekaristi Takatifu na Upatanisho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.