Katibu wa Jimbo la Papa, Kardinali Pietro Parolin, mapema Jumapili iliyopita aliwasili nchini Bulgaria, ambako aliongoza liturujia ya kutabaruku Kanisa Kuu la Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni, ambalo ni Sehemu ya Makao Makuu ya Kitume nchini Bulgaria. Katika homilia yake, Kardinali aliutumia muda huo kufikisha salaam za upendo kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, ambaye kwa moyo mkuu hufuatilia maisha ya Jumuiya ya Wakatoliki nchini Bulgaria, ambayo ingawa ni ndogo, lakini ni hai.
Kwenye tukio hili, Kardinali Parolin, amehimiza Wakatoliki wa Bulgaria kuendelea kuiweka hai roho ya Watakatifu Cyril na Methodi, pamoja na kudumisha udugu na Waotodosi na wito wa kukaribisha waamini wa imani nyingine hata wale wasiokuwa na uhusiano nao wowote wa kidini. Aliwakumbusha umuhimu wa kufanya hivyo hasa katika Mwaka huu wa huruma, na hasa umuhimu kujali kuhudumia maskini wa maskini na walio katika mateso na wanyonge. Aidha Kardinali alikumbuka kwamba katika kanisa hilo pia alitolea sala zake kwa mara ya kwanza, mjumbe wa Kitume wa kwanza nchini Bulgaria, Askofu Mkuu Angelo Roncalli ambaye baadaye alichaguliwa kuwa Papa na kuchagua jina la Papa Yohane XXIII - na pia amemtaja Papa Yohane Paulo II, aliyesisita umuhimu wa kudumisha maisha ya mashahidi Bulgaria, Askofu Yevgeny Bosilkov na Mapadre watatu wa Shirika la Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni ”Assumptionists” waliopigwa risasi wakati wa Ukomunisti.
Katibu wa Jimbo la Papa, Kardinali Pietro Parolin, mwishoni mwa hotuba yake ya kutabaruku hilo Kanisa Kuu, alilikabidhi chini ya usimamizi na ulinzi wa Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni..
Kanisa hilo lililojengwa katika miaka ya 1924, ambalo limefanyiwa ukarabati , lilikuwa halijawahi wekwa wakfu ila kubarikiwa tu. Hivyo Jumapili iliyopita Kardinali Kardinali Parolin, aliliweka Wakfu katika Ibada ya Misa aliyoiongoza akisaidiana na Mjumbe wa Kitume wa Papa , Askofu Mkuu Anselmo Guido Pecorari, pia Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Bulgarian, Askofu Mkuu Christo Proykov, na Maaskofu wengine wawili Katoliki. Katika Ibada hii alikuwepo pia Askofu Mkuu wa Antonio wa Kanisa la Kiotodosi, Msimamizi wa Kanisa hilo katika eneo la Ulaya Magharibi. Miongoni mwa wawakilishi wa serikali, alikuwepo Rais wa Bunge la Bulgaria Tsetska Tsatcheva, Makamu wa Rais wa Jamhuri, Margarita Popova, na Naibu Waziri Mkuu Premier, Meglena Kuneva.
All the contents on this site are copyrighted ©. |