2016-03-20 08:28:00

Yesu ni ufunuo wa sura ya huruma na upendo wa Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko ameanza maadhimisho ya Juma kuu linalomfunulia mwanadamu huruma ya Mungu kwa maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, Kanisa linapokumbuka Siku ile Yesu alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe. Watoto wa Wayahudi wakatandaza nguo zao na kumshangilia Yesu! Hii ni Siku ya XXXI na Vijana  Duniani inayoongozwa na kauli mbiu “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema”. Ni kutokana na umuhimu huu, vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wamekusanyika mjini Roma, ili kumzunguka Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Vijana wakati huu kwa ngazi ya Kijimbo!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake anasema, umati mkubwa wa watu ulimpokea Yesu alipokuwa akiingia mjini Yerusalem huku ukipiga kelele na kusema, ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana! Hivi ndivyo walivyofanya vijana walivyoshuhudia furaha yao ya kumpokea Kristo anayekuja kati ya watu wake; anatamani kuingia katika miji, lakini zaidi katika maisha ya kila mwamini. Yesu anakuja kwa unyenyekevu mkuu pasi na makuu; lakini akiwa na nguvu ya Kimungu inayosamehe dhambi za binadamu na kumpatanisha na Mungu, jirani na nafsi ya kila mmoja!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yesu alifurahia sangwe na vifijo vilivyooneshwa na watu mbele yake! Hakuna jambo lolote linaloweza kumzuia mwamini kushindwa kupata chemchemi ya furaha na amani ya kweli kutoka kwa Kristo, kwani ni Yesu peke yake anayeweza kumkomboa mwanadamu kutoka katika mitego ya dhambi, mauti, wasi wasi na majonzi moyoni! Lakini Liturujia inawakumbusha waamini kwamba, Yesu hakuwakomboa wanadamu kwa kuingia Yerusalemu kwa shangwe, bali alijishusha na kujinyenyekeza, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa mwanadamu.

Yesu alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, Mwana wa Mungu, akawa mwana wa mwanadamu, ili kuonesha upendo na mshikamano na binadamu mdhambi. Hakujionesha kuwa ni Mfalme bali mtumwa aliyejinyenyekesha upeo, ujumbe unaofumbatwa katika maadhimisho ya Juma kuu, Kanisa linapofanya kumbukumbu ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, ushuhuda wa upendo wa hali ya juu, ulioneshwa na Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu alipowaosha mitume wake miguu! Hivi ndivyo walivyokuwa wanafanya watumwa, changamoto kwa waamini kuonesha upendo wa hali ya juu kwa Kristo Yesu na kumwachia nafasi ili naye aweze kuonesha upendo wake kwao, ili kushuhudia upendo wa dhati unaomwilishwa katika huduma makini!

Unyenyekevu wa Yesu unajionesha hata pale alipouzwa kwa vipande thelathini vya fedha! Akasalitiwa na busu la yule mtume aliyekuwa amemchagua kama rafiki. Mitume hawa ambao walionesha ukaribu na Yesu, wakajikuta wametimka na kupotelea mbali kabisa na uso wa Yesu. Petro mtume, akaonesha ujasiri na kumfuasa Kristo nyuma ya njia ya Msalaba! Lakini, udhaifu wa binadamu unamshinda kiasi hata cha kumkana Yesu mara tatu! Yesu ananyanyaswa kwa mateso, kejeli na matusi, hatimaye, anavikwa taji la miiba kichwani na mwili wake wote unaenea madonda na damu tupu! Anahukumiwa kifo, hata kama hakutenda kosa! Pilato anamwona kuwa hana hatia, lakini bado anakuhukumiwa kifo, kwani hakuna mtu ambaye anataka kuwajibika kuhusu hatima ya maisha yake!

Umati mkubwa wa watu uliokuwa unamshangilia Yesu alipokuwa anaingia Yerusalemu, unageuka na kuanza kumzomea na kumshutumu, wakitaka Pilato amfungulie Baraba, mtu aliyesababisha fitina na mauaji, aachiwe huru na Yesu asiye na hatia anahukumiwa kifo! Hivi ndivyo Yesu alivyopitia mateso hata kufa kifo cha Msalaba, adhabu ambayo ilikuwa inatolewa kwa wahaini, watumwa na wauaji wakatili. Yesu akaonja upweke, nyanyaso na mateso, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha sadaka yake iliyopelekea kuyamimina maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa mwandamu!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yesu katika mateso yake alijidhaminisha kwa Baba yake wa mbinguni kwa kusema, “Baba mikononi mwako naiweka roho yangu”! Yesu akawa na nguvu ya kukabiliana na changamoto na kishawishi cha kumtaka kushuka kutoka Msalabani; ashinde ubaya kwa nguvu; aoneshe uso wa mungu mwenye nguvu aliyeshindikana.

Lakini, Yesu anafikia kilele cha sadaka yake kwa kushuhudia na kuonesha sura ya Mungu, mwingi wa huruma; anayethubutu kusamehe na kumfungulia mlango wa Paradiso  mwizi aliyetubu na kukimbilia huruma ya Mungu; ni sura ya Mungu anayegusa sakafu ya moyo wa akida! Hiki ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo na huruma ya Mungu inayoangaza giza; huruma inayojikita katika maisha dhidi ya kifo; huruma inayopandikiza upendo dhidi ya chuki na uhasama!

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, Mwenyezi Mungu anakuja kuwakomboa, wanaitwa kuambata njia yake; njia inayojikita katika huduma, sadaka na majitoleo binafsi. Huu ni mwaliko kwa waamini kusimama na kuangalia Msalaba, darasa la Mungu, ili kujifunza upendo unaojikita katika fadhila ya unyenyekevu; upendo unaokoa na kupandikiza maisha ili kupambana na: ubinafsi, uchu wa madaraka na utukufu wa mambo ya kidunia. Kwa njia ya unyenyekevu wake, Yesu anawaalika wafuasi wake kumfuasa, tayari kumwangalia na kumwomba ili awasaidie kulifahamu Fumbo la sadaka yake! Waamini waendelee kulitafakari Fumbo hili katika hali ya ukimya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.