2016-03-20 08:58:00

Papa Francisko atinga kwenye mtandao wa Instagram!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wa Bikira Maria, Jumamosi, tarehe 19 Machi 2016 amezindua akaunti mpya ya picha kwenye mtandao wa Instagram; mtandao wenye mvuto mkubwa kwa vijana wa kizazi kipya. Akaunti yake inakwenda kwa jina la @ Franciscus. Huu ni mtandao unaomwezesha Baba Mtakatifu Francisko kuwashirikisha vijana wanaogelea katika mitandao ya kijamii kuona baadhi ya picha, lengo ni kuvuka vikwazo vya lugha, ili kuwafikia watu wengi zaidi kwa njia ya lugha ya picha, inayoweza kueleweka na watu wengi zaidi!

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema, matumizi ya mtandao wa Instagram ni hija mpya anayopenda kuitumia, ili kutembea na vijana katika njia ya huruma na upendo wa Mungu. Itakumbukwa kwamba, mtandao wa kijamii wa Instagram ulizinduliwa kwa mara ya kwanza kunako mwaka 2010. Huu ni mtando unaojihusisha na picha peke yake.

Baba Mtakatifu Francisko amezindua matumizi ya mtandao huu mjini Vatican kwa kurusha picha yake ya kwanza inayomwonesha akisali. Tukio hili limehudhuriwa na kushuhudiwa na Bwana Kevin Systrom, Mwakilishi mkazi na mwanzilishi mwenza wa mtandao wa Instagram pamoja na Monsinyo Lucio Adrian Ruiz, Katibu mkuu wa Sekretarieyi ya Mawasiliano mjini Vatican.

Monsinyo Dario E. Viganò, Mwenyekiti wa Sektretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican anasema, kitengo cha mawasiliano ya jamii katika Sektretarieti hii, kitawajjibika kuratibu akaunti ya Baba Mtakatifu Francisko katika mtandao wa kijamii wa Instagram, hasa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Mtandao huu utatumika pia kuwashirikisha vijana wa kizazi kipya picha na video fupi za Baba Mtakatifu Francisko.

Tarehe 19 Machi, ni siku muhimu katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko, kwani hii ndiyo ile siku alipoanza kutekeleza dhamana na utume wake rasmi kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii inatokana na ukweli kwamba, Baba Mtakatifu ana ibada maalum kwa Mtakatifu Yosefu, Mlinzi wa Mwokozi na Msimamizi wa Familia Takatifu. Mtakatifu Yosefu ni msimamizi wa Kanisa zima. Instagram inapania kuwa ni Albam ya picha za Baba Mtakatifu Francisko kwa sasa na wakati mwingine, picha hizi zitaambatana na maneno machache.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.