2016-03-20 09:36:00

Mchakato wa kumwilisha huduma ya upendo katika shughuli za kichungaji


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika tamko lake baada ya mkutano wake wa mwanzo wa mwaka kuhitimishwa huko Jimbo kuu la Genova, kaskazini mwa Italia, linasema, sasa ni wakati wa kumwilisha huduma ya upendo katika mikakati na shughuli za kichungaji nchini Italia. Hiki ni kipindi cha wongofu, kinachowataka Wakleri kuwa na mwelekeo mpya katika utekelezaji wa shughuli zao za kichungaji. Huu ni ufafanuzi ambao umetolewa hivi karibuni na Askofu Nunzio Galantino, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia wakati akizungumza na waandishi wa habari!

Mkutano huu umekuwa ni sehemu ya mchakato wa maandalizi ya mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia utakaofanyika mjini Roma na kuhudhuriwa pia na Baba Mtakatifu Francisko, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu ataufungua mkutano huu ambao kwa namna ya pekee, utakijikita katika upyaisho wa maisha ya Wakleri mintarafu majiundo makini; Ubaba wa Maaskofu na udugu wa Wakleri; maisha ya kiroho na huduma ya upendo katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji.

Majiundo makini yanalenga kuwasaidia wakleri kutambua na kuthamini wito na dhamana yao katika maisha na utume wa Kanisa. Wakleri wanapaswa kushuhudia katika maneno na maisha yao, huduma ya upendo kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya. Hapa majiundo makini yanapaswa kusisitizwa tangu seminari ndogo; kuwa na vigezo muhimu kwa ajili ya vijana wanaotaka kujisadaka katika maisha na utume wa Kipadre.

Ili kuweza kuwafunda majandokasisi wema na watakatifu, kuna haja kwa Kanisa nchini Italia pia kuwekeza katika majiundo makini ya walezi na walimu wa Seminari na nyumba za malezi. Maaskofu watahimizwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa huduma kwa wakleri wao, ili waweze kutenda kadiri ya huruma na mfano wa Kristo Mchungaji mwema. Lengo kuu ni kumwilisha upendo wa dhati katika huduma za kichungaji zinazotolewa na Mama Kanisa nchini Italia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika taarifa yake kwa vyombo vya habari linasema kwamba, kuna haja ya kuwa na busara, kiasi na unyenyekevu katika kushughulikia changamoto ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao Barani Ulaya badala ya kutumia changamoto hii kama tishio la usalama wa wananchi, kama sehemu ya kampeni za uchaguzi! Kuna watu wanaoteseka na kuuwawa huko Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini; hawa ni watu wanaohitaji kuoneshwa mshikamano wa upendo, ili kupewa hifadhi ya kimataifa.

Maaskofu wanasikitishwa na ubaguzi wa kitaifa unaofanywa dhidi ya wakimbizi na wahamiaji Barani Ulaya. Hadi wakati huu, taasisi za Kanisa zinaendelea kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji wapatao 20, 000. Huu ni mchango wa Kanisa Katoliki katika huduma ya upendo kwa wakimbizi na wahamiaji. Maaskofu wanakaza kusema, kuna haja ya kuwa na mfumo maalum unaoratibu na kusimamia mfuko wa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji; kwa kuimarisha ukweli na uwazi; tija na ufanisi si tu katika masuala ya kisiasa, hata pia kwa upande wa Kanisa. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limeamua kwamba, kuanzia tarehe 26 hadi 29 Oktoba 2017 kutaadhimishwa Juma la Kijamii la Waamini wa Kanisa Katoliki Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.