2016-03-20 10:10:00

Endesheni chaguzi zinazojikita katika ukweli na uwazi!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati, CERAC linawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, mchakato wa chaguzi mbali mbali zinazoendelea kufanyika huko Afrika ya kati zinazingatia kanuni maadili, ukweli, uwazi, uhuru, haki na amani; mambo msingi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu katoliki Afrika ya Kati limehitimisha mkutano wake wa mwanzo wa mwaka uliokuwa unafanyika huko Brazzaville.

Maaskofu wanawapongeza wananchi wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kwa kufanya na kuhitimisha mchakato wa uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu, mfano bora wa kuigwa katika kukuza na kudumisha misingi ya ukweli, haki na demokrasia Barani Afrika. Kwa namna ya pekee kabisa wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko aliyeonesha ushupavu wa imani hata akathubutu kwenda Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, ili kuwaimarisha ndugu zake katika mchakato wa haki, amani na maridhiano, tayari kuambata huruma na upendo wa Mungu kwa kuzindua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kati ya watu waliokuwa wanateseka na kukata tamaa kutokana na kinzani pamoja na mipasuko ya kijamii!

Maaskofu wanakaza kusema, kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, ukosefu wa fursa za ajira na umaskini wa hali na kipato; kuna dalili za uvunjifu wa misingi ya haki, amani na maridhiano, mambo ambayo yanahatarisha amani, usalama na mafungamano ya kijamii huko Cameroon, Chad, Congo, Gabon na Equatoria Guinea. Hapa Maaskofu wanasema, kuna haja ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Chaguzi ziwe ni kipimo cha ukomavu wa kidemokrasia Barani Afrika na kwamba, chaguzi hizi ziwe huru na za haki!

Maaskofu wanawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kujisadaka katika kukuza na kudumisha huruma inayojikita katika uhalisia wa maisha ya watu, kielelezo cha imani tendaji! Watu wawe na ujasiri wa kusamehe na kusahau; waanzishe mchakato wa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao, ili kweli Bara la Afrika liweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Maaskofu wanawakumbusha wanasiasa na viongozi wa Serikali kwamba, siasa ni jukwaa la huduma makini kwa wananchi na wala si mahali pa kutafutia ujiko! Si mahali pa kuchuma mali kwa njia za rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma; si mahali pa kulipizana kisasi katika masuala ya kisiasa, bali mahali pa haki, amani, upatanisho, ustawi na maendeleo ya wengi! Siasa ni kwa ajili ya ustawi wa watu na wala si kwa ajili ya mafao binafsi, uchu wa mali na madaraka! Viongozi wenye mwelekeo wa namna hii, wamepoteza dira na mwelekeo wa kisiasa! Wanapaswa kubadilika, au kuachia ngazi ya madaraka kwani siasa si uwanja wao!

Na Padre Richard A, Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.