2016-03-19 06:48:00

Yametimia! Kilele cha huruma ya Mungu kwa mwanadamu!


Ndugu zangu “lala salama” katika mchezo ni zile dakika za mwisho. Hapo timu hutupatia picha ya mchezo ulivyokuwa. Kipenga cha mwisho ndicho kinamtambulisha mshindi. Kadhalika maisha ni lala salama ya kudumu. Mshindi anajulika kinapopulizwa kipenga cha mwisho wa maisha. Leo tuone lala salama ya Yesu na wosia aliotuachia wa kuishi vizuri lala salama ya maisha yetu. Kila mwinjili anasimulia matukio ya dakika za mwisho za maisha ya Yesu kwa namna yake. Malengo yao siyo ya kihistoria, bali ni kutufahamisha jinsi Yesu alivyoishi maisha yake ya upendo na kuyaweka kwa ufupisho dakika za lala salama. Leo tunampata Luka ndiye anayetusimulia upendo wa Yesu akitomasa vipengee vya pekee ambavyo Wainjili wengine hawavigusi kabisa.

Mosi, Yesu alisema: fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” Yesu hakumaanisha kurudia tu tendo hilo kiliturujia, bali alitaka pia kuweka kwa muhtasari maisha yake kwa kujifanya chakula cha maisha ya uzima wa milele. Sisi turudie kitendo hicho yaani, tuwe mkate kwa ajili ya wengine. Kipengee cha pili kinahusu ukuu. “Yakatokea mashindano kati yao, kwamba ni nani anayehesabiwa kuwa mkubwa. Akawaambia,“aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye. Mimi kati yenu ni kama atumikaye.” Tabia ya kuwania ukuu imetiwa ndani mwetu na Mungu mwenyewe.

Hatuna budi kujihoji na kuchagua moja au mwono wa kibinadamu wa kuwania ukuu, au mwono wa Yesu wa kushuka na kutumikia wengine. Sote tungetegemea katika mazingira haya ya chakula na ya kuwekwa Ekaristi Takatifu, mazungumzo yangejikita kwenye kuweka mikakati ya kutekeleza sera za Yesu za kuwa mkate (Ekaristi) kwa ajili ya wengine. Kinyume chake linaibuka zogo la kuwania ukuu. Hapa tunaalikwa kufanya tafakari ya kina kabla ya kutoa maamuzi ya Kristo juu ya upendo. Mbinu za kufanikiwa kutoa maamuzi hayo unayakuta katika kipengee kifuatacho.

Kipengee cha tatu ni kusali. “Ombeni ili msiingie majaribuni.” Yesu mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba. Tatizo walilokuwa nalo wanafunzi ni kutoa maamuzi ya kutumikia wengine badala ya kutumikiwa yaani ukubwa. Kwa hiyo dawa ya kushinda kishawishi hicho ni kusali. Katika lala salama ya maisha yake, hata Yesu mwenyewe alikuwa katika mapambano ya kutoa maamuzi mazito, kwani shetani alimwonesha kuwa ameshindwa lakini kumbe katika sala yaani yaani majadiliano na Baba yake wa mbinguni; katika kuunganika na Baba anapata ushindi. Hapa tunaoneshwa mbinu za kumshinda shetani kuwa ni sala. Halafu, “Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.” Katika biblia malaika anaweza kuwa mtu au ufunuo wa moyo au dhamiri yako inayokuvuvia kutambua maana ya maisha. Hiyo ni kama malaika anayekupa nguvu ya kushinda udhaifu wa kibinadamu.

Kipengee cha nne ni kutafakari na kukazana kupambana: “Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, (mapambano) akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka katika nchi. Alipoondoka katika kuomba kwake, akawajia wanafunzi wake, akawakuta wamelala usingizi kwa huzuni. Akamwambia: Ondokeni mkaombe, msije mkaingia majaribuni. Dhiki au huzuni, kwa kigiriki ni agonia na kwa kiingereza ni agony na maana yake halisi ni mashindano, mapambano, mapigano kama yale ya wanariadha. Yesu alipambana nayo kutoka mwanzo wa kazi yake kule jangwani kama dominika ya kwanza ya Kwaresima, yaani mapambano ya kuamua kumfuata shetani au Baba yake. Unaweza tu kufaulu katika mashindano hayo kwa sala ya ndani kabisa kama ile ya Yesu. Hiyo ni lala salama ya kudumu.

Halafu Luka peke yake anasema jasho au hari kama matone ya damu. Wakati wa mashindano mwanariadha hutoka jasho sana. Kadhalika Yesu yuko kwenye mashindano makali sana ya ndani ya akili na moyo hadi anatoka jasho la damu kwani anadhamiria na kufikiria sana. Hata sisi wakati mwingine tunakuwa katika agony inapotubidi kufanya maamuzi magumu yanayoumiza na kutupatia machungu sana. Hasa tunapotakiwa kumsamehe mtu aliyetujeruhi sana hapo tunakuwa katika mapambano makali sana ndani ya mioyo yetu kati ya kusamehe au kulipa kisasi. Kwa hiyo kutoka jasho kutokana na kutafakari sana, maana yake suala la kumshinda mwovu ni suala la kulidhamiria siyo la kulifanyia mzaha. Hiyo ni lala salama ya kudumu.

Baada ya mapambano hayo makali Yesu anafika na kuwakuta wanafunzi wanaolala usingizi kwa huzuni. Hapa Yesu hawagombezi wanafunzi wala Petro pale alipowakuta wamelala, badala yake anawaona hawaelewi uzito wa kipindi cha lala salama kipindi cha patashika nguo kuchanika hapa ni kusuka au kunyoa!, labda sababu ya udhaifu wa kibinadamu. Lakini anajua wanampenda licha ya udhaifu wao, kwa hiyo anabaki kuwaonea huruma na kuwasamehe bure!. Hapa wanaonywa wachungaji wote kuwa wawasamehe bure na kuwaonea huruma wakosefu na wadhaifu wote, kwamba wanapenda dini lakini ni wadhaifu Ndiyo maana katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha viongozi wa Kanisa kuonesha ile sura ya huruma ya Mungu. Mateso ya Kristo yanaonesha ile sura ya huruma ya Mungu hata kwa wanafunzi wake wanaoelemewa na usingizi wa huzuni. Kadhalika Wainjili wote wanaeleza kwamba wakati wa mateso ya Yesu mitume walimkimbia na Yuda alimsaliti lakini Luka peke yake anasema: “Wote waliojuana naye, na wale wanawake walioandamana naye toka Galilaya, wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo.” (Lk. 23:49).

Kipengee cha tano ni kumtendea wema adui. Kipindi cha lala salama, wachezaji wanaweza kutembeza viatu, kugombana na mchezo ukaisha vibaya. Kwa kikosi cha kutuliza ghasia, maarufu kama FFU, yaani ”Fanya Fujo Uone” hapani mkong’oto tu hadi kieleweke! Angalia lala salama ya Yesu alipofika kushikwa.“Mmoja wao akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. Yesu Akamgusa sikio akamponya.” Wakati wa kumshika Yesu kulikuwa patashika kubwa. Katika vurugu zile mitume walijipanga kujihami. Wakamwuliza Yesu: “Bwana, tuwapige kwa upanga?” Kwa kweli halikuwa swali, bali walitaka tu uhakika waliposema: “Mzee inatosha, katika kesi hii kilichobaki ni kuchomoa majambia na kutembeza visu haiwezekani kufa kikondoo namna hii, lazima tuoneshe kuwa hata sisi tupo!.” Maana yake uovu na maonezi ni kupambana nayo na kurudisha mashambulio. Kumbe, Yesu anafanya kinyume: “Akamgusa sikio akamponya.” Hapa tunafundishwa kuwa mkristu anaweza kuwa na wapinzani lakini hatakiwi kuwa na maadui. Wajibu wa mkristo ni kuwapenda watu wote kwani silaha haimbadilishi adui. Wakristo wajenge utamaduni wa kusamehe na kusahau bila kulipiza kisasi, kwani kisasi ni kazi ya Mungu, mwanadamu hana vigezo sahihi!

Kipengee cha sita: kumhurumia anayekutukana. Katika lala salama ya mchezo kuna kulaumiana na kurushiana matusi. Lakini angalia Yesu anapokanwa na kurushiwa matusi “Bwana akageuka akamtazama Petro.” Wainjili wote wanaonesha jinsi Petro alivyomkana Yesu. Wengine wanadiriki hata kusema kwamba Petro alitoa hata matusi machafu dhidi ya Yesu. Hata hivyo “Bwana akageuka akamtazama Petro.” Neno lililotumika la kigiriki ni emblepo, yaani kutazama kwa undani kabisa kunakogusa dhamiri ya mtu!. Ni sawa na kumwambia Petro kwamba hata kama umenifanya hivyo, mimi najua unanipenda. Ndiyo maana Petro anatoka na kulia! Kilio cha mtu mzima si bure! 

Hapa kuna jambo, amekunwa na ”Jicho la huruma ya Yesu” kama alivyomwangalia yule mwanamke mzinzi, aliyekuwa amehukumiwa kifo!. Hapa tunafundishwa wakristo jinsi ya kuwaona wakosefu, na waovu kwa upendo. Kwani wanaweza kuamsha upendo wa mtu mwovu ukiwaangalia kwa uzuri na wema. Hapa ujumbe ni ”Iweni na huruma kama Baba yenu”! Hii ndugu zangu ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu! Injili ya leo inatupatia muhtasari wa huruma ya Mungu ilivyomwilishwa katika maisha na utume wa Yesu tangu mwanzo hadi kifo chake Msakabani!

Kipengee cha saba ni kudharauliwa. Timu inayoshindwa huzomewa na kutupia mayai mabovu!. Hebu angalia Yesu anavyozomewa. Pilato aliposikia kwamba Yesu ni Mgalilaya akatuma wampeleke kwa Herode Mgalilaya mwenzake. Huyo alikuwa Herode Antipa, mtoto wa Herode mkubwa aliyetafuta kumwua Yesu akiwa mchanga, kiasi cha kutambulika kuwa ”Kizee cha mauaji”. Hebu fuatilia yaliyotokea kwa Herode Antipa: Kwanza“Herode alipomwona Yesu alifurahi sana.” Herode alishasikia kuwa Yesu kuwa maarufu kama mganga wa mazingaombwe! Nadhani wengi mnakikumbuka kile ”Kikombe cha Babu”. Akasubiri kwa hamu sana kukutana naye ili avione ”laivu” vituko vyake. Pili, “Herode akamwuliza Yesu maneno mengi, yeye asimjibu lolote.” Hapo ikaonekana Herode akawa ”amejisapraisi” mwenyewe, akakata tamaa, na mapato yake sasa: “Herode akamfanya duni, pamoja na askari wake, akamdhihaki, na kumvika mavazi mazuri.” Tafsiri yake kigiriki ni kwamba alimchamba na kumwona kama ni mwenda wazimu fulani asiyefaa kwa lolote. Hata wanaomfuata yaonekana walichanganyikiwa. 

Lakini Yesu alikaa kimya hakusema chochote. Hivyo ndivyo inavyomtokea yule anayetegemea kutendewa miujiza na Yesu, anakatishwa tamaa kisha anamdharau. Kwa hiyo ieleweke kuwa ukristo siyo ”supamaketi” au duka la kupata bidhaa, bali ni dini ya utumishi wa upendo; ni dini ambyo imani yake inamwilishwa katika matendo, kielelezo cha imani tendaji! Hi isi dini ya miujiza, wale wanaotaka kuona na kufanyiwa miujiza wana imani haba kama kiatu cha raba!

Kipengee cha nane ni wa mashabiki wa timu iliyoshindwa. Hapa tunawakuta mashabiki wanyonge kwa ajili ya Yesu mnyonge ni wanawake:“Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea.” Ingawaje dhambi wametenda wanaume, lakini wanawake ndio wanaoteseka. Wangesikilizwa zaidi hao, na wanavyoonea huruma pengine vita na maovu ya duniani yangepungua. Kipengee cha tisa. Majeruhi kwenye lala salama hawakosekani. “Leo hii utakuwa pamoja nami peponi.” Mara nyingi Yesu alizugukwa na wadhambi na waovu. Mara ya kwanza alipozaliwa alizungukwa na wachungaji walioeleweka kuwa ni waovu, lakini wakaimbiwa nyimbo na malaika. Sasa yuko msalabani na wevi lakini mmoja anaahidiwa paradisi.

Kipengee cha kumi: Yesu akiwa msalabani anasema. Baba uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.” Wangelijua watendalo wasingelifanya. Yesu hatumii lugha mbaya, bali hutoa maneno ya upendo kwa waovu. Tunaalikwa kuwaangalia vyema wanaokosea badala ya kuwalaani. Tuwe wanafunzi wanaofanya kama mwalimu wao na kusema: “Baba uwasamehe maana hawajui watendalo.” Kwa hiyo lugha na tendo la mwisho kabisa la Yesu ni Huruma na anatuagiza:“Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi.” Jamani, iweni na huruma kama Baba wa mbinguni! Kila jema katika maadhimisho ya kilele cha ufunuo wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu!

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.