2016-03-19 10:31:00

Wekezeni zaidi kwa wasichana na wanawake katika elimu na afya!


Jumuiya ya Kimataifa katika ajenda za maendeleo endelevu kufikia Mwaka 2030, inataka kujikita katika mchakato wa mabadiliko utakaowashirikisha watu wengi zaidi na kwamba, hakuna sababu ya mtu awaye yote kuachwa nje ya mchakato huu. Kutokana na mwelekeo huu, wanawake wanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee, kwa kuwezeshwa na kuthaminiwa kama mawakala muhimu katika maendeleo endelevu!

Nyanyaso, dhuluma na udhalilishaji wa kijinsia unaofanywa dhidi ya wasichana na wanawake; biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; utoaji wa mimba unaokumbatiwa na utamaduni wa kifo; utekaji nyara na wongofu wa lazima pamoja na ndoa za shuruti ni mambo ambayo bado wanatendewa wanawake sehemu mbali mbali za dunia, kiasi cha kubakiza machungu katika miili, akili na mafungamano ya kijamii; mambo ambayo ni uvunjifu wa haki msingi za binadamu!

Huu ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa wakati alipokuwa anachangia kwenye mkutano wa sitini wa Tume ya Wanawake mintarafu ajenda ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030. Katika shughuli zinazotoa tija na uzalishaji, tunu msingi za maisha ya kifamilia zinawekwa rehani; wanawake na wazee wanaachwa pembeni mwa sera na mikakati ya uzalishaji, kiasi cha kuwafanya wajisikie kuwa si mali kitu katika jamii; matokeo yake ni msongo wa mawazo na hatimaye kifo!

Wazee na wanawake wanapaswa kuthaminiwa sanjari na kupewa nafasi ili kuweza kushirikisha uzoefu na mang’amuzi waliyojitwalia katika maisha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jamii husika. Wanawake wajawazito na wale waliojifungua ni kati ya makundi makubwa yanayotengwa katika shughuli za uzalishaji, badala ya kuthaminiwa na kupewa msaada wanaohitaji; matokeo yake ni wanawake kuachwa njia panda kati ya kuchagua kazi au kuwa mama wazazi. Wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa malezi na makuzi ya watoto wao, ndiyo maana ujumbe wa Vatican katika mkutano huu unapenda kuwashukuru na kuwapongeza.

Leo hii katika baadhi ya nchi kuna wanawake na wasichana wanaolazimishwa kukumbatia utamaduni wa kifo kwa kushiriki vitendo vya utoaji mimba au kupachikwa mimba za kupandikiza; matokeo yake, mimba za wasichana ndizo zinazochomolewa zaidi, ikilinganishwa na mimba zinaonesha uhai wa watoto wa kiume. Wasichana wakiwezeshwa kupata elimu bora na makini, watasaidia vyema zaidi majiundo na malezi ya watoto wao; watakuwa na uwezo wa kiuchumi kiasi hata cha kupambana na umaskini, ujinga na maradhi na watakuwa na nafasi kubwa zaidi katika kupanga, kuamua na kutekeleza sera na mikakati mbali mbali ya maendeleo.

Askofu mkuu Auza anasikitika kusema kwamba, katika baadhi ya nchi, huduma ya afya kwa wanawake imetelekezwa na matokeo yake ni athari kubwa kwa afya ya wanafamilia na jamii katika ujumla wake. Utu na heshima ya wanawake vinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Kanisa Katoliki limekuwa mstari wam bele katika kuwekeza kwa wasichana na wanawake kwa njia ya elimu bora na makini inayotolewa kwenye shule, taasisi na vyuo vyake vikuu, vilivyoenea sehemu mbali mbali za dunia. Kanisa liko pia mstari wa mbele katika utoaji wa huduma ya afya kwa wanawake na wasichana.

Askofu mkuu Bernadito Auza anahitimisha mchango wake kwa kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi kwa wanawake na wasichana mintarafu hali yao tayari kushirikiana na kukamilishana na wanaume katika utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo endelevu ya binadamu! Kwa kuwajengea uwezo wanawake, kunasaidia kuimarisha familia nzima ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.