2016-03-19 09:40:00

Mtakatifu Yosefu ni mlinzi wa Mkombozi na Msimamizi wa Familia Takatifu


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican akiwa nchini Macedonia, iliyokuwa Yugoslavia ya zamani Ijumaa, tarehe 18 Machi 2016 ameadhimisha Ibada ya mkesha wa Misa takatifu kwa ajili ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria sanjari na kumbu kumbu ya miaka mitatu tangu Baba Mtakatifu Francisko alipoanza kutekeleza dhamana yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Sherehe ya Mtakatifu Yosefu inawaalika waamini kumwangalia Yosefu mtu wa haki ambaye hakuna mengi yanayosemwa juu yake, lakini alitenda yote katika hali ya unyenyekevu na ukimya mkuu, ili kutekeleza mpango wa Mungu katika kazi ya ukombozi.

Mwinjili Luka anamwonesha Mtakatifu Yosefu kuwa ni mtu wa nyumba ya Daudi, lakini anakaza kuhusu mahangaiko ya Mtakatifu Yosefu alipogundua kwamba, Bikira Maria alikuwa ni mjamzito. Hashindwi na kishawishi na wasi wasi kuhusu hatima ya Bikira Maria, bali anajiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu kwa kumpokea Bikira Maria na Mtoto Yesu maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Yosefu anajitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutekeleza mpango wa ukombozi. Utume wa Yesu, ni kumkomboa mwanadamu kutoka katika lidni la dhambi na mauti!

Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kuhusu umuhimu wa fadhila mbali mbali ambazo Mwenyezi Mungu amewakirimia waja wake kwani wao ni warithi wa utajiri wa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. Zawadi ya imani na fadhila mbali mbali zinafunika uhuru wa waamini, ili kuweza kujiachia mikononi mwa Mungu, tayari kutekeleza mpango na kazi yake ya ukombozi kama alivyofanya Mtakatifu Yosefu. Huyu alikuwa ni mtu wa haki na mwaminifu katika kutii sheria, amri na maagizo ya Mungu.

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume, Redemptoris Custos, uliochapishwa kunako tarehe 15 Agosti 1989 anamtaja Mtakatifu Yosefu kuwa ni Mlinzi wa Mkombozi na Familia Takatifu. Yosefu alikuwa ni mtu mwenye imani thabiti, aliyejiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Mwanadamu anapomweka Mungu pembeni mwa mipango na vipaumbele vya maisha yake, matokeo ni kutumbukia katika majanga yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Wananchi wa Macedonia wamekumbana na magumu katika historia yao, lakini wakathubutu kuyaunganisha na mateso ya Kristo yanayoleta ukombozi kwa mwanadamu!

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, wanajenga maisha yao kwenye mwamba thabiti ambao ni Kristo Yesu, kwa kuonesha imani thabiti inayomwilishwa katika matendo, kielelezo cha imani tendaji! Wakristo wanapaswa kuwa kweli ni watu wema, wakarimu na wenye uwazi; viungo hai vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa unaoshuhudia upendo wa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Kardinali Parolin amewakumbusha waamini umati wa watakatifu kutoka Macedonia, bila kumsahau Mama Theresa wa Calcutta ambaye anatarajiwa kutangazwa kuwa Mtakatifu wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kanisa Katoliki nchini Macedonia halina waamini wengi, lakini linaonesha umoja katika utofauti; upendo na amani inayojikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Baba mmoja!

Wakristo wanahamasishwa kuendelea kukita maisha yao kwa Kristo, mwamba thabiti ili kujenga na kudumisha taifa linalosimikwa katika kanuni maadili; wazi, linalodumisha maridhiano na mshikamano wa kweli kati ya watu wake; mashuhuda na wajenzi utajiri wa maisha ya kiroho na kimaadili, daima wakitamani kutenda mema katika maisha. Kardinali Parolin, amehitimisha mahubiri yake kwa kuiweka familia ya Mungu nchini Macedonia chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu, mume wake Bikira Maria!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.