2016-03-19 15:41:00

Mabalozi wapya wa Vatican: Senegal & Mauritania; Uturuki & Turkmenistan; DRC


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Michael W. Banach kuwa Balozi Mpya wa Vatican nchini Senegal na mwakilishi wa kitume nchini Mauritania. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Michael W. Banach alikuwa ni Balozi wa Vatican huko Papua New Guinea na Visiwa vya Solomon.

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Monsinyo Paul Fitzpatrick Russell, kuwa Balozi mpya wa Vatican huko Uturuki na Turkmenistan. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amempandisha hadhi Monsinyo Russeli kuwa Askofu mkuu. Itakumbukwa kwamba Askofu mteule Russel alizaliwa tarehe 2 Mei 1959 huko Greenfield, Marekani. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa Daraja Takatifu la Upadre hapo tarehe 20 Juni 1987, Jimboni Boston.Alianza utume wake wa kidiplomasia mjini Vatican tarehe 1 Julai 1997. Tangu wakati huo ametekeleza utume wake katika Sekretarieti kuu ya Vatican; akawahudumia kwenye Balozi za Vatican huko Ethiopia, Uturuki, Uswiss, Nigeria na China.

Habari zaidi zinasema, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Monsinyo Francisco Escalante Molina kuwa Balozi Mpya wa Vatican nchini DRC pamoja na kumpandisha hadhi ya kuwa Askofu mkuu. Askofu mkuu mteule Molina alizaliwa tarehe 29 Januari 1965. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa Daraja takatifu la Upadre hapo tarehe 26 Agosti 1989. Tarehe 13 Juni 1998 akajiunga na utume wa kidiplomasia mjini Vatican. Tangu wakati huo, amefanya utume wake kwenye Balozi za Vatican nchini Sudan, Ghana, Malta, Nicaragua, Japan na Slovenia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.