2016-03-18 15:04:00

Umoja wa Wakristo!


Hija kuelekea umoja kamili wa Wakristo baada ya Tamko la Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Majadiliano ya Kiekumene, Unitatis Redintegratio; maadhimisho ya Karne Tano tangu yalipotokea mageuzi ya Kiprotestanti kunako mwaka 1517; changamoto katika ufahamu wa kanuni za Imani na majadiliano katika upendo; ni mambo msingi yaliyopembuliwa na Padre Raniero Cantalamessa mhubiri wa nyumba ya Kipapa wakati wa tafakari yake kwa Baba Mtakatifu Francisko na waandamizi wake, aliyoitoa Ijumaa, tarehe 18 Machi 2016.

Itakumbukwa kwamba, tafakari hizi zimwekuwa ni sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican yalipofanyika. Wakati huu, Padre Cantalamessa anapenda kuchungulia utajiri wa maisha ya kiroho unaofumbatwa katika baadhi ya nyaraka zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Leo anapembua kuhusu Tamko la Majadiliano ya kiekumene na waamini wa Makanisa mbali mbali ya Kikristo na changamoto zake!

Kumekuwepo na maendeleo makubwa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa ya Kikristo tangu baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Waamini wengi wanatamani kuona Kanisa la Mungu linaloonekana na kushuhudia umoja.Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican baada ya kutangaza hati juu ya Kanisa, wakasukumwa na hamu ya kurejesha tena umoja kati ya wafuasi wa Kristo na Mababa wa Mtaguso wakataka kuwaonesha Wakatoliki wote njia, maana na misaada ili waweze kuitikia wito na neema hizi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Huu ukawa ni mwanzo wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Umoja wa Wakaristo ambalo limepewa dhamana ya kushughulikia masuala ya Mafundisho tanzu ya Kanisa. Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, viongozi mbali mbali wa Makanisa ya Kikristo wamekutana na kuzungumza na Mababa Watakatifu, kiasi cha kufungua mwelekeo mpya wa ushirikiano kama ilivyojionesha hivi karibuni kati ya Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima alipokutana na Papa Francisko huko Cuba. Ni mwelekeo unaopania: kusali, kutangaza na kushuhudia Injili kwa pamoja.

Juhudi kama hizi zilioneshwa na Wakristo wa madhehebu mbali mbali kunako mwaka 2009 Wakristo wa Madhehebu mbali mbali walipokusanyika na kusali huko Stockholm, wengi wakaona kuwa hii ilikuwa ni Pentekoste mpya kwa Makanisa! Hawa ni waamini waliokuwa wanamasika kuona umoja wa Kanisa ukishuhudiwa na Wakristo wote, ili kuondoana na tabia ya kuwaona Wakristo wa Makanisa mengine kuwa kama wapinzani na adui, dhana ambayo kwa sasa imepitwa na wakati!

Padre Cantalamessa anakaza kusema, wakristo sehemu mbali mbali za dunia wanajiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya miaka mia tano tangu yalipotokea mageuzi ya Kiprotestanti, lengo ni kulinasua Kanisa na historia ya utengano iliyopota. Leo hii changamoto kubwa ni kuwasaidia watu kutambua dhana ya dhambi na madhara yake katika maisha ya watu! Watu wanahesabiwa haki kwa njia ya imani na neema inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka, kitovu cha imani ya Kanisa inayopaswa kumwilishwa katika maisha ya watu kwa njia ya ushuhuda. Neno la Mungu linapaswa kupewa uzito unaostahili. Tamko kuhusu kuhesabiwa haki liwasaidie Wakristo kuwa na mang’amuzi binafsi kuhusu ukweli huu na changamoto ya kuambata uhuru wa kweli badala ya kuwa ni chachu ya upinzani kati ya wanataalimungu na Makanisa yao!

Kanuni na mafundisho ya Kanisa ni matunda ya mchakato wa maisha ya Wakristo. Kumbe, leo hii bado kuna changamoto ya uelewa kati ya Makanisa kuhusiana na: imani na matendo; Biblia na Mapokeo ya Kanisa. Matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni muhimu sana kwa mwamini kuweza kurithi maisha ya uzima wa milele. Vita na mapambano kati ya  Wakristo ni mambo yaliyopitwa na wakati, sasa ni wakati wa kumwambata Kristo Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima.

Padre Raniero Cantalamessa anakaza kusema, Umoja wa Wakristo unajengwa na kuimarishwa kwa njia ya huduma ya upendo; katika maisha na kazi; katika ukweli na upendo kwani upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari, haujivuni; haukosi kuwa na adabu. Upendo kwa Mungu na jirani ni mambo muhimu sana yanayoshuhudia imani inayomwilishwa katika matendo. Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka yawasaidie Wakristo kuvunjilia mbali kuta za utengano, ili kwa pamoja waweze kujisikia kuwa wamoja katika Roho Mtakatifu, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.