2016-03-18 08:58:00

Rais wa Ureno akutana na Papa Francisko mjini Vatican!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 17 Machi 2016 amekutana na kuzungumza na Rais Marcelo Rebelo de Sousa wa Ureno, ambaye baadaye alikutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Kwa mara ya kwanza Rais De Sousa amefanya ziara ya kikazi tangu alipochaguliwa kuwa Rais wa Ureno; ameonesha kufurahishwa na mahusiano yalipo kati ya Vatican na Ureno sanjari na mchango wa Kanisa katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ureno, hususan katika masuala ya kijamii, maisha, utu, heshima ya binadamu na tunu msingi za maisha ya kifamilia.

Baba Mtakatifu na mgeni wake katika mazungumzo yao, wamegusia pia masuala ya kimataifa na kikanda, hususan hali tete huko Ukanda wa Bahari ya Mediterannia na hali ya Bara la Ulaya katika ujumla wake. Changamoto ya wahamiaji na wakimbizi ni kati ya mambo ya kimataifa yaliyopewa uzito wa pekee wakati wa mazungumzo haya kutokana na hali halisi ilivyo kwa sasa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.