2016-03-18 08:06:00

Dumisheni ukweli, uwazi na uwajibikaji kwa mali ya umma!


Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tomè na Principe, CEAST, baada ya mkutano wake wa mwaka uliohitimishwa hivi karibuni limewataka viongozi wa Serikali na taasisi za umma kuhakikisha kwamba, zinawajibika barabara  kwa kukuza na kudumisha kanuni maadili, uongozi bora; ukweli na uwazi katika matumizi ya rasilimali na fedha ya umma; ili yote haya yasaidie mchakato wa huduma bora kwa wananchi wa Angola.

Maaskofu wanasema, umefika wakati kwa wafanyakazi wa Serikali na taasisi za umma kutumia vyema rasilimali na fedha ya umma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi badala ya mwelekeo wa sasa ambako fedha ya umma inaonekana kuwanufaisha watu wachache ndani ya jamii. Maaskofu wanawaalika wananchi wenye uwezo kiuchumi kuwekeza zaidi katika shughuli za uzalishaji na utoaji huduma, ili kupanua wigo wa fursa za ajira kwa wananchi wengi wa Angola,ili kupambana na ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tomè na Principe linaendelea kuwahimiza waamini na wananchi wote kutokata tamaa kutokana na myumbo wa uchumi kimataifa na kitaifa, kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta ya petroli katika soko la kimataifa. Takwimu zinaonesha kwamba, Angola ni nchi ya pili Barani Afrika kwa uzalishaji wa nishati ya petroli.

Maaskofu wamesikitishwa na takwimu za ongezeko la vifo vya watoto wadogo na wanawake wajawazito nchini Angola sanjari na vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Malaria na Homa ya Njano. Itakumbukwa kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Angola hivi karibuni limetiliana sahihi na Wizara ya Ulinzi, ili Wamissionari waweze kusaidia kutoa huduma ya tiba na kinga kwenye Hospitali za kijeshi nchini humo. Ukame nao unaendelea kuwa ni tishio kwa maisha ya watu na mifugo, mwaliko kwa wananchi wote wa Angola kushikamana katika mapambano dhidi ya kuenea kwa jangwa pamoja na kuwasaidia waathirika wa ukame, ili watu wasipoteze maisha kutokana na baa la njaa!

Maaskofu thelathini wameshiriki katika mkutano huu ambao pamoja na mambo mengine umejadili kuhusu maboresho ya huduma ya Radio Ecclèssia nchini Angola ili iweze kutoa huduma kwa nchi nzima. Imekuwa ni nafasi ya maandalizi ya mkutano wa IMBISA utakaofanyika huko Lesotho mwezi Novemba, 2016 pamoja na maadhimisho ya Kongamano la Kikanisa litakalotimua vumbi mwezi Agosti, katika Jimbo kuu la Huambo, Angola.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.