2016-03-17 09:56:00

Patashika nguo kuchanika Wilayani Chato!


Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato kwa tuhuma za ubadhirifu, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. Watumishi hao ni Mkuu wa Idara ya Kilimo na Ushirika, Bw. Mwita Mirumbe Waryuba pamoja na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya, Bw. Dioniz Mutayoba. Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana usiku, Jumatano, Machi 16, 2016) alipokuwa akizungumza na watumishi wa idara zote na taasisi zilizomo kwenye wilaya ya Chato katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Mshikamano SACCOS wilayani humo.

Afisa Kilimo na Ushirika anadaiwa kuchangisha kiasi cha sh. milioni 20 kutoka kwa watumishi wa Halmashauri hiyo kwa ajili ya kuanzisha SACCOS tangu mwaka 2013 lakini hadi sasa SACCOS haijaanzishwa na wala fedha hizo hazijarejeshwa. Fedha hizo zinadaiwa kuliwa na watumishi watatu (majina yamehifadhiwa). Aidha, Bw. Waryuba anadaiwa kutumia lugha chafu na za vitisho kwa watumishi walio chini yake ikiwa ni pamoja na kuomba na kupokea rushwa, na kunyanyasa na kudhalilisha kijinsia baadhi ya watumishi wa kike.

Inadaiwa pia Bw. Waryuba alikopa bila kufuata taratibu za mikopo wilayani Chato ambapo alikopa sh. milioni 15 kutoka Mwambao SACCOS na sh. milioni 15 nyingine kutoka Chato Teachers’ SACCOS tangu mwaka 2015 na tangu wakati huo hajazirejesha hali ambayo imeleta manung’uniko kutoka kwa viongozi na wananchama wa SACCOS husika. “Malalamiko ya watumishi na wananchi dhidi ya huyu bwana yamefikishwa kwa Kaimu Mkurugenzi lakini hajachukua hatua kwa sababu ni rafiki yake,” alisema Waziri Mkuu. Kaimu Mkurugenzi huyo ni Mhandisi Joel Baha ambaye hakuwepo ukumbini hapo kwa sababu yuko kwenye ziara ya mafunzo huko Japan.

Kwa upande wake, Bw. Mutayoba ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo anadaiwa kuzembea kusimamia mradi wa kufyatua matofali ya gharama nafuu (interlocking bricks) zilizogawiwa kwa vikundi vinne vya vijana wa wilaya hiyo. “Mwaka 2013 Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lilitoa mashine nne za kufyatulia matofali ya bei nafuu kwa ajili ya vikundi vinne vya vijana wilayani Chato. Mashine hizo ziligawiwa kupitia kwa Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya, Bw. Dioniz Mutayoba na kila kikundi kilipewa sh. 500,000 ili waanze kazi ya kufyatua matofali na kuyauza kwa bei nafuu katika maeneo waliyopo lakini hadi leo hakuna kitu kilichofanyika,” inasema sehemu ya taarifa.

Afisa huyo anadaiwa kugawa mashine mbili kwa kila kata katika kata za Muganza na Buseresere lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika kwani vikundi hivyo havikuzalisha kitu chochote tangu wakati huo. Aidha, Bw. Mutayoba anatuhumiwa kudai na kupokea rushwa kwa wanachama wa vikundi vya ujasiriamali ili aweze kuvisaidia kupata mikopo. “Yaani watu wanakuja kukopa sh. milioni mbili halafu unawadai kitu kidogo cha sh. 300,000. Sasa mradi waliotaka kufanya wataweza kuukamilisha kweli?,” alihoji Waziri Mkuu.

“Huyu Bwana amelalamikiwa lakini Mkurugenzi aliyepita naye anadaiwa kumlinda kwa sababu ni rafiki yake,” alisema Waziri Mkuu na kuibua minong’ono ndani ya ukumbi huo. Aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chato, Bw. Clement Berege hivi sasa amehamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba. “Katika Serikali hii tunataka tuwe na Halmashauri zilizo safi. Lakini pia Serikali hii ina mkakati wa kuimarisha ushirika na tunataka kuinua kilimo. Kwa hiyo basi, TAKUKURU na Polisi wachunguzeni hawa watu wawili kwa maana ya Afisa Ushirika na Afisa Maendeleo ya Jamii na nipewe taarifa uchunguzi utakapokamilika,” alisema Waziri Mkuu.

Mapema, akizungumza na watumishi hao, Waziri Mkuu ambaye amewasili mkoani Geita kwa ziara ya siku mbili akitokea mkoani Kagera, alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi hao aliwakumbusha wajibu wao wa kuwahudumia Watanzania bila kujali hali zao na akasisitiza kuwa Serikali haitamuonea mtumishi yeyote ambaye anatimiza wajibu wake. “Napenda kusisitiza kuwa malengo ya Serikali ni kuimarisha utendaji wa watumishi lakini pia Serikali hii haitamvumilia mtu mdanganyifu, mzembe, asiye mwadilifu na mla rushwa. Ukiharibu kazi hapa Chato mwwisho wako ni hapa hapa tu. Usitarajie kupelekwa Bunda au kwingine ili ukaharibu na huko,” aliongeza.

ASIMAMISHWA KAZI KWA KUMDANGANYA WAZIRI MKUU:Ni Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Chato:Pampu yadaiwa kupelekwa Morogoro, yeye asema iko kijijini

Waziri mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Chato, Bw. Peter Ngunura kwa kosa la kumdanganya mbele za watu na kumpa taarifa za uongo juu ya pampu ya maji iliyodaiwa kupelekwa Morogoro. Waziri Mkuu alitoa agizo hilo Jumatano, Machi 16, 2016 alipokuwa akiwahutubia mamia ya wakazi wa mji wa Chato waliojitokeza kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wilayani Chato, mkoani Geita.

Waziri Mkuu ambaye amewasili mkoani Geita kwa ziara ya siku mbili akitokea mkoani Kagera, alisimamishwa na wakazi wa kijiji cha Kalebezo, kata ya Nyamirembe, wilayani Chato na kukuta mabango yaliyokuwa yakidai maji safi na kuelezea uharibifu wa pampu ya maji. Katika maelezo yao, wakazi hao walimweleza Waziri Mkuu kwamba mradi wa maji kwenye kata hiyo ulishakamilika lakini pampu yao imechukuliwa na kupelekwa Morogoro jambo lililosababisha wakose maji kwa muda mrefu. Kwa sababu alikuwa hajafika Chato mjini na hakuwa na taarifa sahihi za mradi huo wa maji, Waziri Mkuu aliwaeleza wakazi hao kwamba analibeba jambo hilo na atafuatilia hadi aelezwe ni kwa nini pampu hiyo imepelekwa Morogoro. Akiwa kwenye mkutano wa hadhara, ndipo suala la maji likaibuka tena na Waziri Mkuu kuamua kuchukua hatua hiyo.

It’s unethical (ni kinyume cha maadili) kumdanganya kiongozi wako. Nimekuuliza mara mbili mbili kama una uhakika kuwa pampu hiyo ipo ukasema una uhakika kuwa ipo. Nimemtuma diwani na vijana wangu wakacheki wakasema hakuna pampu,” alisema Waziri Mkuu na kumwita Diwani huyo jukwaani ili atoe majibu. “Pale kulikuwa na pampu mbili; moja ni ya kuvuta maji kutoka kwenye kina kirefu na kuyapeleka kwenye pump house na nyingine ni ya kuvuta maji kutoka kwenye pump house na kuyapeleka kwenye tenki kubwa la kuhifadhia maji. Ile ya kutoa maji kwenye kina kirefu ndiyo haipo, wataalamu wanajua wameipeleka wapi,” alisema Bw. Charles Manoni ambaye ni diwani wa kata ya Nyamirembe ambayo kijiji cha Kalebezo kimo.

Waziri Mkuu alisema ahadi ya Serikali ya awamu ya Tano ni kuwatumikia wananchi kwa uadilifu. “Lazima watumishi wa umma wabadilike na kuanza kuwatumikia wananchi kwa dhati. Hatuwezi kuwa na watumishi waongo ambao wanamdanganya hata Waziri Mkuu.” “Kuanzia sasa, Engineer atakaa pembeni, Polisi na TAKUKURU wamchunguze. Asitoke Chato hadi uchunguzi ukamilike. Nataka kujua nani alichukua hiyo pampu na kwa kibali gani. Tukijiridhisha atarudi lakini kwa sasa hivi akae kando,” alisema.

Mapema jana mchana, akizungumza na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Geita na wilaya ya Chato mara baada ya kupokea taarifa zao kwenye ukumbi wa Halmashauri, Waziri Mkuu alimpa fursa Mhandisi huyo aeleze nini kimetokea kuhusu pampu inayodaiwa kupelekwa Morogoro lakini akakanusha na kudai kuwa ipo palepale kijijini.

“Una uhakika na hayo unayoyasema? Hiyo pampu ipo kweli kijijini? Nikienda nitaiona?” alihoji Waziri Mkuu na kujibiwa mara mbili na mhandisi huyo kwamba ana uhakika asilimia 100 kwamba pampu ipo na wala haijaenda Morogoro. Alipotaka kujua ni kwa wananchi wa kijiji kile hawana maji kutokana na ubovu wa pampu hiyo, alijibiwa kwamba mradi ule ulikuwa chini ya mamlaka ya maji ya mji wa Bukoba (MBUWASA) ambako wilaya hiyo ilikuwepo zamani kabla ya kuhamishiwa kwenye mkoa mpya wa Geita mwaka 2012. Mhandishi huyo alisema amekuwa akifuatilia fedha za matengenezo kutoka kwa Mkurugenzi wa MBUWASA bila mafanikio, ndipo Waziri Mkuu akamuagiza aende nje ya ukumbi huo akapige simu na kumletea majibu ni lini fedha hizo zitapatikana ili wananchi wa kijiji kile waendelee kupata maji.

Na Ofisi ya Waziri mkuu wa Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.