2016-03-17 15:49:00

Onesheni mshikamano na maskini duniani!


Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza washiriki wa mkutano wa “2016 Havard World Model United Nations” kutoka katika mataifa mbali mbali duniani, kielelezo cha utajiri wa utamaduni wa familia ya binadamu. Kama wanafunzi jukumu lao kubwa ni kutafuta ukweli, maelewano na ukuaji katika hekima kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jamii zao sanjari na kukuza ushirikiano na mshikamano wa kimataifa unaodumishwa kwa miaka mingi.

Miundo mbinu hii ni muhimu sana kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Umoja wa Mataifa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, watakuwa tayari kwa ajili ya huduma na tunza ya miundo mbinu na taasisi kama hizi. Lakini ikumbukwe kwamba, mahusiano ya kidiplomasia, miundo ya kimataifa ni mambo ambayo yanapaswa kupewa msukumo wa pekee na wanafunzi wa kimataifa, lakini muhimu zaidi ni kuhakikisha kwamba wanafunzi hawa wanatumia karama na vipaji vyao ili kukabiliana na changamoto zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kila mwanafunzi anao uzoefu na mang’amuzi ya shida, magumu na changamoto zinazowakabili ndugu zake kutoka katika nchi zao za asili. Ni vyema kwa wakati huu kuendelea kujifunza kutoka kwa wanafunzi wenzao, ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha ya watu. Kuna watu wanaojibidisha usiku na mchana ili kutafuta mahitaji ya watoto wao; kuna watu wanaoteseka kutokana na nyanyaso, dhuluma na ubaguzi; kiasi kwamba, leo hii wamegeuka kuwa ni wakimbizi na wahamiaji; wameacha makazi, ardhi na uhuru wao.

Hawa ndio wale watu wanaohitaji msaada wa wasomi kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa, ili kujenga na kudumisha haki, amani na mshikamano. Mtakatifu Paulo anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufurahi pamoja na wale wanaofurahi; kulia pamoja na wale wanaolia. Nguvu yao kama Jumuiya katika ngazi mbali mbali za kijamii inajikita katika uelewa na uwezo wa mtu binafsi na upendo unaodhihirishwa kwa wengine bila kusahau huduma kwa wale wasioweza kujihudumia wenyewe!

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wanafunzi hawa wamepata walau nafasi ya kuweza kuona shughuli mbali mbali zinazofanywa na Kanisa Katoliki katika kuwahudumia maskini, wakimbizi na wahamiaji; familia na jumuiya sanjari na kusimama kidete kulinda na kutetea utu na haki msingi za wanajumuiya hawa wa familia ya binadamu. Wakristo wanaamini kwamba, wanahamasishwa na Kristo Yesu kuwahudumia jirani zao bila ubaguzi na kwamba, huu ndio wito wa jumla unaosimika mizizi yake katika ubinadamu! Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa wanafunzi hawa na kuwapatia baraka zake za kitume na furaha kwa wale wote wenye kiu na njaa ya haki na wajenzi wa amani duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.