2016-03-17 16:04:00

Matumaini ni fadhila ya maisha ya Kikristo!


Matumaini ni fadhila ya Kikristo inayojikita katika unyenyekevu na nguvu ya kuweza kusonga mbele katika safari ya maisha, licha ya vikwazo na magumu yaliyopo. Matumaini kwa Mwenyezi Mungu kamwe hayawezi kumdanganya mwamini kwani Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu katika kutekeleza ahadi zake. Mungu ni chemchemi ya furaha na amani mioyoni mwa waja wake. Haya ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 17 Machi 2016 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican.

Yesu alipokuwa anazungumza na walimu wa sheria aliwakumbusha kwamba, Abraham alikuwa na furaha kubwa katika matumaini ya kuonana na Yesu siku moja katika maisha yake. Hii inaonesha kwamba, matumaini ni nguzo muhimu sana katika maisha ya Wakristo. Abrahamu, Baba wa imani alikutana na changamoto na vizingiti katika safari yake ya imani, lakini akaamini, akamtumainia na kumtii Mwenyezi Mungu, akiwa njiani kuelekea kwenye Nchi ya ahadi iliyojaa maziwa na asali.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, matumaini ni fadhila inayounganisha historia nzima ya wokovu na hii ni chemchemi ya furaha ya kweli. Kanisa linahubiri kuhusu furaha inayojikita katika matumaini na kwamba, Mtakatifu Paulo anazungumzia matumaini yaliyokuwa yanakwenda kinyume cha matumaini, anapomwangalia Abrahamu, Baba wa imani. Matumaini, unyenyekevu na hali ya kawaida vinamwezesha mtu kupata furaha inayomwezesha kusonga mbele pasi na makuu, kwa kumpatia amani, usalama na kwamba, haya ni matumaini yasiyodanganya kamwe!

Baba Mtakatifu anafafanua zaidi kwamba, hii ndiyo iliyokuwa ile furaha ya Abrahamu, Baba wa imani, iliyoendelea kukua na kukomaa katika historia ya wokovu! Wakati mwingine furaha hii ilimezwa kiasi hata ikashindwa kuonekana kama ilivyojidhihirisha kwa Elizabeth aliporuka kwa furaha, siku ile alipotembelewa na binadamu yake Bikira Maria. Hiki ni kielelezo cha furaha inayobubujika kutokana na uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Fadhila ya matumaini ni chemchemi ya furaha na amani iliyojionesha hata wakati ule Waisraeli walipokuwa utumwani Misri! Matumaini kamwe hayawezi kumdanganya mtu!

Mwenyezi Mungu alizungumza na Abraham una hatimaye, akazungumza na Yesu; changamoto kubwa mbele ya waamini wengi ni kwamba ni rahisi sana kuwa na imani na mapendo, lakini ni vigumu kuwa na fadhila ya matumaini kwani hii ni fadhila inayomwandama mwanadamu katika maisha yake ya kila siku bila kumwacha azame na kupotea katika bahari ya shida na magumu ya maisha. Matumaini ni nguvu inayotenda katika hali ya ukimya, inajikita katika unyenyekevu, lakini ni kielelezo cha nguvu ya ndani. Hivi ndivyo alivyoshuhudia Yesu kwa njia ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wake! Matumaini yanaunganisha historia na maisha ya wakristo wote! Anasema Baba Mtakatifu Francisko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.