2016-03-16 08:25:00

Mwaka wa Huruma Jimbo Katoliki Musoma!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni fursa makini kwa waamini kumtafakari Kristo; uso wa huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Huruma ni kitovu cha maisha ya Kikristo na daraja linalomuunganisha binadamu na Muumba wake. Ni mwaka ambao waamini wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kutoka kimasomaso kushuhudia huruma, wema na upole wa Mungu kwa jirani zao, kielelezo cha uwepo endelevu wa Ufalme wa Mungu kati ya binadamu.

Maandiko Matakatifu yanaonesha kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo na wala si mwepesi wa hasira. Huruma ya Mungu ni ufunuo wa upendo wa Mungu kwa binadamu uliooneshwa kwa namna ya pekee na Kristo Yesu katika maisha yake ya hadhara, kwani aliwaponya watu na mapungufu yao ya kibinadamu; akawaondolea dhambi na hivyo kuwaweka huru. Aliwaangalia watu kwa jicho la upole na upendo, wakaguswa, wakatubu na kumwongokea Mungu. Hii ni changamoto ya kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata huruma yake isiyokuwa na mipaka.

Ikumbukwe kwamba, huruma ni sehemu ya vinasaba na uhai wa Kanisa; kumbe, waamini wanaalikwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu katika maisha yao, hususan wakati huu, Kanisa linapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hii ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma wakati wa kuzindua Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu Jimbo Katoliki Musoma. Waamini wanaalikwa kuambata huruma ya Mungu kila mara wanapoingia na kutoka Kanisa kwa kupitia Lango la huruma ya Mungu.

Ili kupata rehema inayotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, waamini wanapaswa kuwa karibu na Mungu kwa njia ya toba na wongofu wa ndani. Wawe pia wepesi kuwaonjesha jirani zao huruma inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake; kwa kuomba na kutoa msamaha kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu na Baba mwenye huruma aliyekuwa tayari kumsamehe mtoto wake hata baada ya “kutumbua” mali yake na “makahaba wa mji”.

Mwenyezi Mungu anasamehe na kusahau, lakini mwamini hana budi kupiga moyo konde kwa kutubu na kukimbilia huruma ya Mungu. Waamini wawe karibu zaidi na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, Sala, Tafakari ya Neno la Mungu pamoja na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Askofu Msonganzila anawaalika waamini kujibidisha zaidi kuitafuta na kuiambata huruma ya Mungu katika maisha yao, kwani wameumbwa na Mungu bila ridhaa yao, lakini hawezi kuwakomboa bila ya wao kujishughulisha kikamilifu.

Lengo kuu ni kumfikia Mwenyezi Mungu kwa kufanya matendo mema; kwa kuwa na huruma kwani huruma ni kipimo cha maisha na maadili. Wanandoa waoneshane huruma na upendo, ili ndoa zao ziweze kudumu na kuzaa matunda ya utakatifu. Wakristo wanaoishi uchumba sugu, iwe ni fursa ya kurekebisha maisha yao, ili kukaribisha huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Familia iwe ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya huruma na msamaha; haki, amani na upendo.

Kwa njia hii, kweli familia zitaweza kuonesha sura ya huruma ya Mungu kwa jirani zao, lengo kuu la Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Wapadre na watawa wawe kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa watu wao kwa njia ya huduma makini na sadaka ya maisha yao ya kila siku! Ndivyo anavyosema Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma.

Na Veronica Modest,

Musoma.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.