2016-03-16 10:30:00

Msikate tamaa Mungu atawafariji!


Huruma na faraja ni tema ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameitafakari wakati wa katekesi yake Jumatano, tarehe 16 Machi 2016 kwa kufanya rejea kwenye Kitabu cha Nabii Yeremia, Sura ya thelathini na thelathini na moja; sehemu hii ya Maandiko Matakatifu inaitwa "Kitabu cha faraja”, kwani hapa huruma ya Mungu inajionesha katika uwezo wake wote wa kufariji na kufungua mioyo iliyopondeka tayari kuambata matumaini mapya katika safari ya maisha ya kiroho. Itakumbukwa kwamba, hii ni katekesi endelevu kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Waisraeli walikabiliwa na uchungu mzito wakati walipokuwa uhamishoni; tukio ambalo liligusa na kutikisa msingi wa imani yao. Nabii Yeremia anawakumbusha Waisraeli kwamba, kamwe Mwenyezi Mungu hajawasahau watu wake kwani atageuza masikitiko yao kuwa furaha; Mwenyezi Mungu atawafariji na kuwafurahisha ili waache huzuni zao; atawaonesha upendo na kuwakomboa. Haya ni maneno ya faraja kwa watu wengi duniani wanaoendelea kukabiliana na maafa pamoja na majanga mbali mbali ya maisha.

Baba Mtakatifu anaendelea kukaza, matukio yote haya bado yanaendelea kuonesha wema na huruma ya Mungu inayowaalika waamini kutubu na kumwongokea Mungu, ili waweze kupata huruma na msamaha wake; changamoto ya kuwa na mwanzo mpya. Mwenyezi Mungu anawaahidia watu wake kupata neema hata wakiwa jangwani; watafurahia matunda ya kazi zao; badala ya maombolezo watapata faraja. Nguvu ya Mungu itaonesha uweza mkuu kwa kuchipua maisha kutoka katika kifo na neema kutoka katika maovu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, unabii wa Yeremia unapata utimilifu wake kwa ujio wa Kristo Yesu, ambaye Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wake unatangaza na kushuhudia ukuu wa huruma ya upendo wa Mungu na utekelezaji wa ahadi ya upatanisho, upyaisho na maisha ya uzima wa milele. Wakati huu, waamini wanapoendelea na hija ya maisha ya kiroho kuelekea maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, Baba Mtakatifu anawaalika kwa namna ya pekee kukimbilia kwenye kiti cha huruma ya Mungu, ili waweze kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao na hapo wataonja huruma, amani na furaha ya kweli!

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni kipindi cha neema na upyaisho wa maisha ya kiroho! Hakuna sababu ya watu kukata wala kukatishwa tamaa, kwani Mungu daima yuko pamoja nao, mwaliko wa kutafuta uwepo na huruma ya Mungu, ili aweze kuwafariji. Waendelee kujenga na kudumisha urafiki na Mwenyezi Mungu.

Hata katika shida na mahangaiko mbali mbali yanayoweza kuleta mashaka mioyoni mwa waamini, lakini ukweli ni kwamba: Mwenyezi Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake na chemchemi ya matumaini hata kama watapita katika bonde la uvuli wa mauti, hawana sababu ya kuogopa! Baba Mtakatifu Francisko ameungana kwa namna ya pekee na vijana Jimbo kuu la Cracovia wanaosherehekea Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kutafakari kuhusu “Vijana na Huruma”. Vijana hawa wanapopita katika Lango la Huruma ya Mungu; wanaposhiriki katika maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho; Wanapoabudu Ekaristi Takatifu na kutafakari Injili ya Msamaria mwema, wapige moyo konde, tayari kumfuasa Kristo Yesu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anawaalika vijana kutoka Poland kujiandaa kuwakaribisha vijana wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia watakaokwenda nchini humo kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya thelathini na moja ya Vijana Duniani. Baba Mtakatifu anawataka vijana hawa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.