2016-03-16 14:50:00

Msalaba ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu!


Dominika ya Matawi au kama inavyojulikana kwa jina lingine “Dominika ya Mateso ya Bwana” inatuingiza katika Juma Kuu kipindi ambacho Kanisa linafikia kilele cha kipindi cha Kwaresma kwa kuadhimisha Mafumbo makuu ya ukombozi wetu, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Dominika hii  inaunganisha maadhimisho mawili makubwa: Kwanza ni kumbukumbu ya kuingia kwa shangwe Bwana wetu Yesu Kristo Yerusalemu huku akishangiliwa kama mfalme wa Wayahudi na pili ni maadhimisho ya Mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo.

Ni adhimisho ambalo linatuweka katika njia panda: ni kwa vipi leo hii huyu anayeshangiliwa kama mfalme kama masiha anageukwa na kunuiwa kwamba auwawe? Kwa ujumla Dominika hii inalifunua fumbo zima la Upendo mkuu wa Mungu ambao ni mkuu kuliko uovu wa mwanadamu. Dhambi haishahabiani na utukufu wa Mungu. Utukufu wake na ufalme wake si katika uovu wa ulimwengu huu bali katika kumtukuza Mwenyezi Mungu. Ni vema basi kuzitafakari sura zote hizo mbili kama pande mbili za sarafu kusudi tuweze kuingia vema katika Juma hili kuu na kupata matunda sahihi yatokanayo na fumbo zima la Pasaka.

Kwanza tuione furaha ya watu wa Yerusalemu kwa ujio wa Kristo kwao kama Mfalme. Furaha yao inasababishwa na hali ya kijamii na kisiasa ambamo wao kama taifa wamo. Kipindi kile Israeli kama mataifa mengine walikuwa chini ya utawala wa warumi. Hamu yao kubwa ilikuwa ni ujio wa masiha ambaye atakuja kuwatoa katika utumwa huo. Hamu hii haikutokea hewani tu. Walitiwa matumaini na maandiko matakatifu na hivyo Kristo alipojitambulisha kwao kama masiha basi waliona mwanzo mpya umefika. Sehemu ya pili ya adhimisho la leo inatupeleka katika mapinduzi ya Kristo ambayo yanamsababishia aingie katika mateso. Ni wazi kwamba maisha yake yote ya hadharani alijaribu kuwaeleza wafuasi wake juu ya utumwa halisi ambao unapaswa kuondolewa. Huo ni utumwa wa dhambi ambao unatuondoa katika kuhusiana na mwenyezi Mungu. Fumbo la Msalaba linafunua huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu.

Tunaweza vipi basi kuunganisha hali hizi mbili za mateso na utukufu wa ufalme wa Mungu? Hapa ningependa tuutafakari ufalme wa Mungu kwa kina kidogo, ili kuweza kutambua maana yake katika maisha yetu wanadamu. Kama tunakavyotafakari Siku ya Ijumaa Kuu, Kristo anaeleza wazi kwamba ufalme wake si wa dunia hii. “Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa wayahudi”. Hapa Kristo anaeleza wazi kwamba yeye anao ufalme, lakini ni ufalme ambao namna yake haipaswi kusawazishwa na namna ya falme za kidunia, haupaswi kusawazishwa na mbwembwe, mabavu na kupenda ubwana kunakofanywa na viongozi wa dunia hii. Kristo mbele ya Pilato anaufafanua ufalme wake kuwa ni wa namna gani. Anasema: “Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya nimekuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli huisikia sauti yangu”. Ni ufafanuzi wa aina ya ufalme wake kwa upande mmoja lakini pia ni mwaliko wa kusikia sauti yake ili kukaa katika hiyo kweli na hapo ndipo tunaweza tukamshangilia kama mfalme. Hii ni namna ya kutofautisha fikra za Wayahudi ambao wanampokea kama masiha wakisema: “ndiye mbarikiwa mfalme ajaye kwa jina la Bwana”.

Tunaweza kuangalia maeneo kadhaa katika Biblia mbapo Kristo alionesha wazi kupingana na utukufu wa kibinadamu na namna ambavyo wayahudi walimtambulisha vibaya Mungu. Mfano baada ya kulisha watu wengi kwa mikate michache walitaka kumfanya mfalme ila Krsito alipingana nao mara moja (Rej Yoh 6: 14 – 15, 26 – 27). Hata wakati wa majaribu ya shetani habari ambayo tuliitafakari mwanzoni mwa kipindi hiki cha Kwaresima Kristo alipingana waziwazi na utukufu wa kidunia (Mt 4: 5 – 10). Yote haya yanatuonya ili tuwe makini na namna dhambi inavyotuvuta na kujitafuta sisi wenyewe na ufahari wetu na kumtupilia mbali mwenyezi Mungu na maagizo yake.

Hapa ndipo tunaiona athari kubwa ya dhambi kwetu sisi wanadamu yaani kututoa katika uwepo wa Mungu na kuishi si katika ukweli bali katika namna ya utumwa wa shetani. Utumwa huo ndiyo unatufanya kupoteza upendo kati yetu na kuwa na matabaka. Hali hiyo ndiyo inatupeleka katika uhalisia wa kimaisha wa kuwa na watawala na watawaliwa. Hivi havitufikishi katika amani na uelewano bali daima hutuingiza katika mapigano, mafarakano na kila mmoja kutafuta kupambana ili kuwa bora zaidi ya mwingine. Hivi ndivyo hutuondoa katika hali ya kuwa kama ndugu. Kila mmoja hupambana si kwa ajili ya ufanisi wa jamii nzima bali ni kwa ajili ya manufaa yake binafsi. Katika hali hii kamwe hatuwezi kuuona upendo wa Mungu ambao ndiyo unadhihirisha utawala wake kwetu.

Hali hii ndiyo inatupasa kutuelekeza tumpokee vipi masiha na katika namna gani. Yeye anatufundisha namna iliyo njema ya kuutawadha ufalme wa Mungu hapa duniani. Daima ni kuisikiliza sauti ya Mungu na kukabidhi yote kwa Mungu. “Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu”. Hadi hatua ya mwisho ya maisha yake Kristo anajikabidhisha kwa Mungu. Hili linawezeshwa na ukubali wake wa kujishusha ili Mungu atawale kama Mtume Paulo anavyotuambia katika somo la pili ya Dominika hii akisema: “alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa ... alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba”.

Unyenyekevu utufanya kuwa waaminifu kwa kazi ya Mungu. Nabii Isaya analikazia hilo katika somo la kwanza. “Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma”. Lakini pia anaendelea kuelezea kuwa tunakuwa wanyenyekevu kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Mungu sababu Yeye mwenyewe ndiye atakayetutegemeza katika kuustawisha ufalme wake: “kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya”.

Unyenyekevu wa Kristo unajionesha katika namna ya juu kabisa pale Msalabani. Huyu ambaye pale katika maji ya mto Yordani alitamkwa na Mungu kama “Mwanangu mpendwa” (Mt 3:17) na pia Kayafa alimpatia sifa ya kifalme (Mt 26:63 – 67) alihitajika kuonesha ukuu wake. Wakuu wa Mafarisayo walimdhiaki wakisema: “Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu mteule wake “Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi ujiokoe mwenyewe”. Hii ni dhiaka kutoka kwa maaskari waliomsulubisha. Lakini pia hata waliosulubiwa naye walimjaribu: “Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi”. Ni wakati mgumu ambao Kristo alitarajiwa katika sifa na fahari za kibinadamu kudhihirisha ukuu wake”. Lakini Yeye alijibu kwa utulivu na unyenyekevu.

Leo hii tunaonywa kuepa kukumbatia dini kama kitu kitakachotupatia maslahi binafsi, utukufu na fahari za kidunia. Unaweza kuingia katika hatari ya kumchangamkia Kristo na hata kumtumikia lakini si katika misingi ile ya kikristo, misingi aliyoiweka ambayo kwayo ndiyo inaujenga ufalme wake. Tunaweza kujikuta tunaitwa wakristo ambao tunaimba nyimbo nzuri za kumsifu Mungu lakini hatuuishi ukristo. Leo hii unapomtukuza na kumfurahia kuwa ni mwana wa Daudi, Mfalme ajaye kwa jina la Bwana, anakualika pia kuustawisha ufalme huo hata kama ulimwengu utakukataa na kukufanya kupita katika mateso. Ni katika njia hiyo ya msalaba ambapo mwanadamu amepokea dharau yote, amepokea namna zote za kukataliwa, amepokea madhulum ya namna yote, lakini ndipo hapo Mwenyezi Mungu anapoionesha hekima yake ya ajabu na nguvu zake.

Hivyo ninakualika katika adhimisho la Dominika ya leo kumpokea kwa shangwe Kristo anayekuja kwako akiwa amepanda punda, mnyama dhaifu kabisa ambaye hastahili kutumiwa na mfalme, ishara ya unyenyekevu wake na ufunuo wa ufalme wake kwetu. Anakujia leo akitaka umpokee kwa shangwe na kumuinulia matawi na kumuita Yeye Mfalme. Ni kweli, Yeye ni Mfalme, anakuja kutuletea ufalme ambao nabii Isaya aliagua tangu kuzaliwa kwake kwamba “uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; naye ataitwa jina lake, mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani”. Huyu ndiye mbarikwa ajaye kwa jina la Bwana, mfalme wa Israeli.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.