2016-03-16 08:03:00

Mahujaji millioni 3 wametembelea Vatican!


Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji mpya, ambalo limepewa dhamana ya kuratibu na kusimamia maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anasema, tangu kuzinduliwa kwa maadhimisho haya, takribani mahujaji millioni tatu wametembelea na kusali kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Askofu mkuu Fisichella ameyasema haya, Jumatatu tarehe 14 Machi 2016 wakati akizungumza na waandishi wa habari ili kuelezea mwenendo mzima wa maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu, maadhimisho ambayo yamewagusa wengi, hasa kutokana na changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko ya kutubu na kuongoka, ili kuambata huruma ya Mungu inayomwilishwa pia katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili!

Dr. Franco Gabrielli, msimamizi wa Jiji la Roma ameshiriki pia katika mkutano huu na waandishi wa habari. Taarifa zinazonesha kwamba, nusu ya mahujaji waliofika hapa mjini Roma wameshiriki katika matukio mbali mbali ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu Jimbo kuu la Roma.Takwimu zinaonesha kwamba, kuna maelfu ya waamini ambao wanaendelea kupitia Lango la Huruma ya Mungu kwa Makanisa yaliyotengwa kwa ajili ya hija ya Mwaka Mtakatifu mjini Roma na kwenye Makanisa mahalia sehemu mbali mbali za dunia. Kwa kuwa hii ni Jubilei ya watu wote wa Mungu kadiri ya uwezo na nafasi zao.

Askofu mkuu Fisichella amewashukuru viongozi wa Serikali ya Italia pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kufanikisha mchakato wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa amani na utulivu. Haya ni mazingira ambayo yanawawezesha waamini na mahujaji kusali na kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa amani na utulivu wa ndani. Inakadiriwa kwamba, idadi ya mahujaji wanaokuja mjini Roma itaendelea kuongezeka siku hadi siku kadiri ya matukio mbali mbali yaliyoko kwenye Kalenda ya maadhimisho haya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.