2016-03-16 15:05:00

Fungeni na kusali ili kuombea amani nchini Syria


Chama cha Kitume cha Pax Christi, kuanzia tarehe 15 hadi 20 Machi, 2016 kinawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kufunga kwa ajili ya kuombea amani nchini Syria ambayo kwa muda wa miaka mitano imekuwa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoungwa mkono na mataifa makubwa, kila taifa likiwa linatafuta masilahi yake katika mgogoro huu.

Pax Christi linamwalika mtu mmoja mmoja na makundi ya watu kuonesha mshikamano wa dhati kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria ambao kwa kiasi kikubwa wameathirika kutokana na vita, ili cheche za matumaini zilizoanza kujionesha ziweze kuzaa matunda ya amani ya kudumu nchini Syria. Vita nchini Syria ilianza kunako mwezi Machi, 2011, watu wakata uhuru na haki zao msingi kuheshimiwa, lakini kwa bahati mbaya, wakakumbana na mkono wa chuma, hali ambayo imepelekea madhara makubwa huko Mashariki ya Kati.

Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha miaka mitano ya vita watu zaidi 250, 000 wameuwawa kikatili. Zaidi ya watu millioni 13.5 wanahitaji msaada wa dharura nchini Syria. Watu millioni 6.5 hawana makazi ya kudumu wala huduma msingi. Kuna wananchi millioni 4.6 kutoka Syria ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao na sasa wanatangatanga kutafuta hifadhi na usalama wa maisha katika nchi jirani.

Ikumbukwe kwamba, kuna maelfu ya wakimbizi pia kutoka Palestina na Iraq ambao hawapaswi kusahaulika pia kwani wanakumbana na hali ngumu ya maisha kwa sasa. Haya ni makundi ya wananchi wanaoendelea kutafuta haki kwa msaada wa Jumuiya ya Kimataifa. Kuna kila dalili kwamba, vita hii haitaweza kumalizika mapema iwezekanavyo Pax Christi inasema. Lakini kuna haja ya kuokoa maisha ya watu kwa kusitisha mashambulizi na kutoa ulinzi na usalama kwa raia na mali zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.