2016-03-15 16:48:00

Askofu Agapitus Nfon anakuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo la Kumba!


Baba Mtakatifu Francisko ameunda Jimbo Jipya la Kumba nchini Cameroon kwa kuligawa Jimbo la Buèa na hivyo kulifanya kuwa ni sehemu ya Jimbo kuu la Bamenda. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Askofu Agapitus Enuyehnyoh Nfon,  kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki Kumba ambaye hadi kuteuliwa kwake alikuwa ni Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bamenda, Cameroon.

Jimbo Katoliki la Buèa kabla ya kumegwa kwake lilikuwa na eneo la kilometa za mraba 13, 524 baada ya kumegwa sasa lina Kmq 2, 093. Jimbo Katoliki la Kumba litakuwa na Kmq 11, 431. Jimbo Katoliki la Buèa lilikuwa na wakazi wapatao 1, 120, 000 sasa litakuwa na wakazi 557, 854 na Jimbo Jipya la Kumba litakuwa na wakazi 562, 988. Jimbo Katoliki la Buèa litakuwa na Wakatoliki 203, 617 na Jimbo Katoliki la Kumba litakuwa na Wakatoliki 205, 491.

Jimbo Katoliki la Buèa litakuwa na Parokia 19 wakati Jimbo Katoliki la Kumba litakuwa na Parokia 16. Mapadre Jimbo Katoliki la Buèa ni 53 wakati Mapadre Jimbo Katoliki la Kumba ni 33. Watawa ni 112 na Makatekista ni 197 kwa Jimbo Katoliki la Buèa na Jimbo Katoliki Kumba litakuwa na Watawa 44 na Makatekista 182. Kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu, Parokia ya Fiango litakuwa ni Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Kumba kuanzia sasa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.