2016-03-14 07:23:00

Simameni kidete kulinda ndoa kadiri ya mpango wa Mungu!


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Tamko lao kuhusu Kanisa na Ulimwengu, Gaudium et Spes linazungumzia pamoja na mambo mengine baadhi ya masuala yanayohitaji kufafanuliwa upesi, ili kustawisha heshima ya ndoa na ya familia, kwa kuangalia kwa kina na mapana ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo; utakatifu wa ndoa na familia; upendo wa ndoa; uzazi katika ndoa; kupatana kwa upendo wa ndoa na heshima ya uhai wa binadamu na kwamba, ustawiwa ndoa na familia unapaswa kushughuliwa na wote!

Haya ni mambo msingi ambayo yamepewa kipaumbele cha pekee na Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri mkuu wa nyumba ya Kipapa wakati wa tafakari yake ya Kipindi cha Kwaresima kwa waandamizi wa Baba Mtakatifu, Ijumaa tarehe 11 Machi 2016. Padre Cantalamessa anakaza kusema, kuna haja kwa waamini kusimama kidete ili kurejesha tena ule mpango asili wa Mungu kwa binadamu unaojikita katika mahusiano ya dhati kati ya bwana na bibi. Kwa bahati mbaya, tendo la ndoa limechafuliwa kiasi kwamba, Shetani hataki kuona waamini wakijikita katika mpango wa kazi ya uumbaji kadiri ya utashi wa Mungu.

Padre Cantalamessa anasema, Maandiko Matakatifu kutoka Agano la Kale yanaonesha mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu unaopata hitimisho lake kwa kushiriki kikamilifu katika kazi ya uumbaji, kwa mwanaume kuungana na mke wake na matunda ya muungano huu ni watoto ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Daima mwanaume amekuwa ni tabia ya kujiona sana kiasi hata cha kushindwa kumpokea vyema mwenzi wake wa maisha. Hii ni changamoto ya kuwa wazi na kumpokea mwenza wa maisha, tayari kupokea na kushiriki katika mpango wa Mungu kwa mwanadamu.

Ndoa inabubujika kutoka katika fadhila ya unyenyekevu inayowakumbusha wanandoa kwamba, wanategemeana na kukamilishana katika hija ya maisha yao ya pamoja. Bwana na bibi wakipendana wanapaswa kushuhudia unyenyekevu wa hali ya juu kabisa na hii inakuwa ni shule ya kwanza ya maisha ya kidini. Mwenyezi Mungu katika mpango wake aliwaumba wote sawa, lakini kwa bahati mbaya ndoa ikageuka kuwa ni kielelezo cha mfumo dume na mwanamke akaonekana kuwa mnyonge zaidi mbele ya mwanaume.

Padre Cantalamessa anakaza kusema, Wimbo Ulio Bora unarejesha tena ule uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa, alama ya Agano kati ya Mungu na mwanadamu, inayoshuhudiwa katika fadhila ya upendo wa dhati, uaminifu, udumifu; sifa ambazo zimeonesha mahusiano kati ya Mungu na Waisraeli katika historia ya wokovu. Yesu Kristo akayapatia mahusiano kati ya mwanaume na mwanamke hadhi ya Sakramenti, yaani alama ya uwepo wa neema ya Mungu kati ya waja wake!

Kwa bahati mbaya anasema Padre Cantalamessa leo hii kuna mkanganyiko mkubwa kuhusu maisha ya ndoa na familia, kiasi hata cha majadiliano haya kutaka kung’oa uwepo wa Mungu ambaye ni chanzo cha uwepo wa mradi huu. Leo hii ndoa na familia inapigwa “madongo na kutiwa mchanga kiasi cha kuonekana kuwa si mali kitu”! Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wameonesha na kushuhudia uzuri na utakatifu wa ndoa inayojengwa kati ya bwana na bibi na matunda na muungano huu ni watoto wanaopaswa kulelewa vyema. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akafafanua kwa kina na mapana kuhusu upendo wa kimungu, yaani “Agape” na wala sio ule wa kujisikia katika vionjo yaani “Eros” katika Waraka wake wa Kitume, Mungu ni upendo, “Deus caritas est”.

Padre Cantalamessa anasema, waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema wanapaswa kusimama kidete kupambana na kile kinachoitwa kwa Umombo “Gender Revolution” mageuzi ya kijinsia yanayotaka kufuta tofauti za kijinsia zilizopo kati ya mume na mke! Hapa waamini wanachangamotishwa kurejea tena katika mpango wa Mungu kwa binadamu kama unavyosimuliwa na Maandiko Matakatifu, kwa kuungama na kushuhudia Injili ya familia mintarafu Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ndoa inapaswa kuonekana kuwa ni zawadi ya hali ya juu kati ya bwana na bibi!

Mwishoni, Padre Cantalamessa anawashauri watu waliokwekwa wakfu pamoja na wanandoa kusaidiana katika mchakato wa kujengana; huku kila upande ukijifunza kutoka kwa wengine ili kuheshimu na kukumbatia mpango na utume wa Mungu kwa kila kundi! Ukarimu, maisha ya sadaka, huduma makini kwa Injili ya uhai ni muhimu sana kama kielelezo cha ushuhuda wa Injili; mambo ambayo leo hii katika ulimwengu mamboleo yanaonekana kuwa hayana thamani hata kidogo! Lakini ni muhimu mbele ya macho ya Mwenyezi Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.