2016-03-14 15:28:00

Papa Francisko analaani mashambulizi ya kigaidi huko Pwani ya Pembe!


Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika huko Grand-Bassam, Jumapili tarehe 13 Machi 2016 na kusababisha vifo vya watu kumi na sita na kati yao kuna askari wa wawili. Baba Mtakatifu anaungana na wananchi wote wa Pwani ya Pembe kulaani mashambulizi haya yanayoendelea kupandikiza chuki na uhasama kati ya watu.

Hayo yamo kwenye ujumbe ulioandikwa kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu Raymond Ahoua, F.D.P. wa Jimbo Katoliki Grand-Bassam. Baba Mtakatifu anapenda kutoa salam zake za rambi rambi kwa familia zilizofikwa na msiba huu mzito. Anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa majeruhi, ili waweze kupona haraka na kurejea tena katika shughuli zao. Anaziombea roho za marehemu huruma ya Mungu, mwanga wa milele na pumziko la amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.